MPINA AMDHARAU SPIKA WA BUNGE.

Taarifa ya Spika Leo

Katika Kikao cha 40 cha Bunge, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, alitoa mchango akieleza kuwa kampuni na viwanda vya sukari nchini vilivyopewa dhamana na Serikali ya kuhakikisha kunakuwa na sukari ya kutosha vimeshindwa kutekeleza wajibu huo. Aliongeza kuwa kushindwa huko kwao kumesababisha upungufu wa sukari nchini na hivyo kusababisha bei ya sukari kupanda hadi kufikia TSh 10,000 kwa kilo moja.

Mbunge, Mhe. Mpina, alitoa hoja akidai kuwa Waziri huyo analidanganya Bunge na kwamba viwanda havijashindwa kutimiza wajibu wao, bali serikali imeshindwa kushirikiana vema na viwanda na kampuni hizo katika kuingiza sukari nchini.

Mhe. Mpina alipewa muda wa kutoa ushahidi ambao, kwa mujibu wa kanuni, alipaswa kuuwasilisha kwa Spika ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kushughulikia ushahidi kwa madai yoyote ya kusema uongo Bungeni.

Spika alisema kwamba kabla hajachukua hatua yoyote, alihitaji kujiridhisha na ushahidi wa Mhe. Mpina ama kuupeleka kwenye kamati ili uchambuliwe na kujiridhisha kisha ilete taarifa ya mwisho kwake. Hata hivyo, Mhe. Mpina aliitisha mkutano na waandishi wa habari, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni na taratibu za Bunge. Mpina amekuwa mbunge tangu mwaka 2005, hivyo ni mbunge mzoefu anayezifahamu ipasavyo sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza Bunge.

Spika alisema kuwa kitendo kilichofanywa na Mhe. Mpina ni cha utovu wa nidhamu kwa Bunge zima na kwa Spika. Aliongeza kuwa ni kitendo cha kudharau mamlaka ya Spika, kuingilia mwenendo wa Bunge, na kushusha hadhi na heshima ya Bunge.

Kifungu cha 26 (d) cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kinazuia kitendo cha kumkosea heshima Spika kwa maneno ama matendo. Kifungu cha 26 (a) kinazuia vitendo vya dharau kwa shughuli za Bunge, na kifungu cha 34 (1)(g) kinazuia kuchapisha kwa umma taarifa zilizoandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuwasilishwa Bungeni pasipo kibali cha Bunge na kabla ya taarifa hizo kuwekwa mezani.

Kitendo cha Mhe. Mpina kinakwenda kinyume na vifungu hivi vya Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge.

Spika ameongeza kuwa baada ya kujiridhisha, ameona kwamba Mhe. Mpina amemkosea na kulikosea Bunge. Hii ni kwa sababu amejipa mamlaka ya kibunge ambayo hayana msingi. Hivyo, sheria zinampa mamlaka Spika kutoa hukumu kwa mbunge mwenye matendo ya namna hii.

Maelekezo ya Spika:

1. Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge ikutane kujadili jambo hili la Mhe. Mpina na kutoa maoni na mapendekezo kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Bunge.

2. Ushahidi uliowasilishwa pia umekabidhiwa kwa kamati hiyo upitiwe na kutoa maoni kama ni wa kweli ama la.

3. Taarifa iwasilishwe Jumatatu, tarehe 24 kwa Spika.

Maswali na Mashaka kuhusu Hoja za Mhe. Mpina

Baada ya maelezo haya, ni muhimu kujiuliza ni kitu gani kimemsukuma Mhe. Mpina kutumia vyombo vya habari kutoa wazi ushahidi huu huku akijua ni nje ya utaratibu wa kanuni na sheria za Bunge. Moja, ya mambo yanayotia mashaka ni hoja za Mhe. Mpina kwenye jambo hili kwani inaonekana wazi anatumia nafasi yake Bungeni kuwasaidia ma cartel wa sukari kwa kuzuia juhudi za serikali za kushughulikia tatizo la sukari nchini.

Hii inaashiria kuwa Mhe Mpina yupo kwenye kundi moja linalopinga muswada wa NFRA ambao unalenga kuruhusu serikali kununua na kusambaza sukari, hatua ambayo ingeweza kumaliza utegemezi wa Watanzania kwa wasambazaji wa sukari nchini. Kwa kufanya hivyo, Mhe. Mpina anatia hofu umma wa watanzania na kuonesha viashilia vya kushirikiana na wauzaji wa sukari ambao wamekuwa wakiendelea kudhibiti soko la sukari na kupandisha bei kiholela kwa faida yao binafsi.

Hii itaendelea kuwaumiza Watanzania wa kawaida ambao wanakumbana na bei ya juu ya sukari na uhaba wa bidhaa hiyo muhimu huku wakitumia fedha nyingi kuzuia mapendekezo mapya ya sheria ambayo yanawezesha serikali kununua na kusambaza sukari kupitia taasisi ya serikali NFRA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *