RAIS SAMIA ATOA HAKIKISHO LA USHIRIKI WA WAKAZI WA NGORONGORO KATIKA UCHAGUZI.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa uhakikisho kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, utafanyika kama ilivyopangwa.

Rais Samia amesisitiza kuwa mipaka ya vijiji na vitongoji katika maeneo hayo itazingatiwa kama ilivyokuwa awali.

Kwa niaba ya Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. William Lukuvi, akizungumza na wananchi wa kata 11 za Tarafa ya Ngorongoro leo Ijumaa, Agosti 23, 2024.

Amewahakikishia kuwa serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa haki na uwazi. Pia, amewaagiza askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuepuka unyanyasaji dhidi ya wananchi na kuheshimu mamlaka za serikali za mitaa, akiongeza kuwa Rais Samia anathamini uwepo wa serikali za vijiji na vitongoji katika maeneo hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, kwa upande wake, aliwashukuru wananchi kwa subira yao na imani waliyonayo kwa serikali. Aliahidi kufuata maagizo yote yaliyotolewa, hususan kuhakikisha huduma za kijamii, kama vile afya na elimu, ambazo zilikuwa zimesimama au kulegea, zinarejeshwa kwa ubora unaotakiwa.

Ziara ya Mhe. Lukuvi pia ilihudhuriwa na viongozi wengine wa ngazi za juu, wakiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, CP Awadh Juma Haji, pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika hotuba yake, Mhe. Lukuvi alisisitiza kuwa kila diwani anatakiwa kufikisha ujumbe wa Rais kwa wananchi katika kata zao. “Ni muhimu wananchi waelezwe kwamba hakuna aliyezuia kupiga kura; Rais ameagiza wananchi wote wapige kura kama kawaida,” alisema Lukuvi.

Mhe. Lukuvi pia alieleza kuwa Rais Samia amepokea ujumbe uliokuwa kwenye mabango yaliyobebwa na wananchi, na ameahidi kupanga siku na mahali pa kukutana na wawakilishi wa jamii ya Ngorongoro ili waweze kumweleza Rais moja kwa moja masuala yao.

Mwisho, Waziri Lukuvi alitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro, akisema, “Nina habari kuwa baadhi ya huduma hazitolewi vizuri. Ninaagiza kuhakikisha huduma zote zinarejeshwa kikamilifu, kwani Rais anawapenda watu wake na anataka kuona wananchi wanapata huduma bora kama ilivyokuwa awali.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *