Aliyekuwa Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mjumbe wa Kamati Kuu kwa miaka mingi, Rostam Aziz, ameibuka hadharani na kumkosoa vikali aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, akimtuhumu kwa kukosa historia ya uanachama na kutokuwa na uhalali wa kuikosoa CCM.

Akizungumza katika mahojiano maalum kupitia runinga ya Azam TV, Rostam amesema kuwa Polepole hana uzoefu ndani ya CCM na hajawahi kushika nafasi yoyote ya kiuongozi kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Kwa kweli, sijawahi hata kusikia jina lake kabla ya mwaka 2015. Hajawahi kushika nafasi yoyote ya kiuongozi ndani ya chama, na ghafla tu akateuliwa kuwa katibu mwenezi. Kwa mtu kama huyo, siwezi kumpa hadhi ya kuzungumzia historia, utamaduni, mila wala utaratibu wa CCM,” alisema Rostam kwa msisitizo.

Rostam amesisitiza kuwa mtu ambaye hana mizizi wala mchango ndani ya chama hawezi kuwa sauti ya mabadiliko au kukosoa taasisi hiyo. Amesema hatua ya Polepole kuhoji maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Taifa ni sawa na kudharau mamlaka ya juu kabisa ya chama na viongozi wote waliokuwepo.
“Kiongozi anayebeza Mkutano Mkuu wa CCM, anawadharau wajumbe wote walioketi katika mkutano huo, pamoja na viongozi waliokaa meza kuu. Huyo si kiongozi wa itikadi, bali ni wa maslahi binafsi,” aliongeza.
Rostam pia amemshutumu Polepole kwa kutokuwa mfano wa kuendeleza demokrasia ndani ya chama wakati alipokuwa katika nafasi ya katibu wa itikadi na uenezi, akisema kuwa alitumia nafasi hiyo kwa masilahi binafsi badala ya kusimamia maadili na misingi ya chama.
Amewataka wanachama wa CCM kutompa uzito Polepole kwa maoni yake, kwa kuwa historia yake ndani ya chama haimpi mamlaka ya kutoa mwelekeo wa chama hicho kongwe barani Afrika.
Katika hatua nyingine, Rostam ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa aliyoifanya tangu achukue madaraka mwaka 2021.
“Rais Samia amerejesha uchumi kwenye mstari, amejenga shule nyingi, hospitali na zahanati kuliko rais yeyote kabla yake. Ameendeleza miradi aliyoirithi na kuanzisha mipya, huku akifungua milango ya uwekezaji na biashara,” amesema Rostam.
Ameeleza kuwa uongozi wa Dkt. Samia umeboresha mazingira ya biashara, kuongeza bajeti ya umwagiliaji, na kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia wananchi wa maeneo ya vijijini kupitia ujenzi wa barabara na usambazaji wa umeme katika kila kijini.
Rostam amewataka Watanzania kumrejesha Rais Samia madarakani kwa muhula mwingine wa miaka mitano ili nchi ipige hatua zaidi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Tukimpa tena miaka mitano, Tanzania itapiga hatua kubwa mno. Wanaompinga hawana hoja, bali ni chuki na wivu wa maendeleo,” amehitimisha.