Na Mwandishi Wetu
Tangu kuingia madarakani mwaka 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonyesha uongozi unaoegemea katika misingi ya usawa, ustawi na maendeleo jumuishi. Katika kipindi cha miaka minne tu, maamuzi na mageuzi aliyoyatekeleza yamegusa moja kwa moja maisha ya Watanzania wa kipato cha chini, hasa wale wanaoishi vijijini na wanaojitahidi kuinua familia zao kupitia kilimo, ufugaji, elimu na ajira ndogo ndogo.

Ifuatayo ni orodha ya maamuzi 20 muhimu yanayothibitisha kuwa Serikali ya Dkt. Samia ni serikali ya wanyonge:
1. Kuongeza Idadi ya Wanafunzi Wanaopata Mikopo ya Elimu ya Juu
Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu kutoka 142,000 mwaka 2021 hadi 248,000 mwaka 2024, hatua inayowezesha watoto kutoka familia masikini kuendelea na masomo bila vikwazo vya kifedha.

2. Ujenzi wa Barabara Vijijini
Mtandao wa barabara vijijini umeongezeka kutoka km 108,000 mwaka 2021 hadi km 144,000 mwaka 2024, ongezeko la zaidi ya 25%. Maendeleo haya yamefungua fursa za masoko, huduma na ajira vijijini ambako ndiko chanzo cha umasikini wa wengi.
3. Kulipa Deni la Mifuko ya Wafanyakazi
Dkt. Samia aliamua kulipa zaidi ya Tsh trilioni 2 kwa mifuko ya hifadhi ya jamii, deni lililodumu kwa zaidi ya robo karne. Uamuzi huu umeimarisha ustawi wa wastaafu na kulinda haki za wafanyakazi.

4. Kuongeza Vyuo vya Elimu ya Kati
Vyuo vya elimu ya kati vimeongezeka kutoka 640 mwaka 2021 hadi 860 mwaka 2024, hatua inayotoa nafasi kwa vijana wengi wa kimasikini kupata ujuzi na ajira.
5. Kuboresha Mafao ya Wastaafu
Fomula ya mafao imeboreshwa kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40 ya mkupuo, ikiwa ni hatua ya kihistoria ya kupunguza kilio cha muda mrefu cha watumishi wa umma.
6. Kuimarisha Sekta ya Madini
Viwanda vya kuchakata madini vimeongezeka kutoka 2 hadi 9 ndani ya miaka minne, na kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania, wakiwemo wachimbaji wadogo.
7. Kukuza Viwanda vya Vyama vya Ushirika
Viwanda vya vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka 2 hadi 7, hatua inayowezesha wafugaji kupata soko la uhakika la mazao yao kama ngozi na maziwa.

8. Kupeleka Umeme Vijijini
Zaidi ya vijiji 2,000 vimepatiwa umeme, na kufanikisha malengo ya kufikia vijiji vyote nchini. Umeme umeleta mapinduzi ya uzalishaji na huduma katika maeneo ya vijijini.
9. Kiwanda cha Mbolea Dodoma
Kiwanda cha kuzalisha mbolea tani milioni 1 kwa mwaka kimeanzishwa Dodoma, hatua inayochochea kilimo cha kisasa na kupunguza gharama kwa wakulima wadogo.
10. Mikopo Midogo kwa Wajasiriamali
Zaidi ya Tsh trilioni 3.6 zimetolewa kupitia TASAF, SELF na manispaa mbalimbali kusaidia wajasiriamali wadogo kiwango kikubwa kuliko awamu yoyote ya nyuma.
11. Kuongeza Ufadhili kwa Kaya Masikini
Bajeti ya TASAF kwa kaya masikini imeongezeka kutoka Tsh 500 bilioni hadi 980 bilioni, ikionyesha dhamira ya kupunguza umasikini kwa vitendo.

12. Kuongeza Vituo vya Afya
Vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka 8,700 hadi 12,800, na huduma za upasuaji sasa zinapatikana hadi ngazi ya kata jambo lililopunguza gharama na vifo.
13. Kuongeza Bajeti ya Barabara za Changarawe
Ujenzi wa barabara za changarawe umeongezeka kutoka 24,000 km mwaka 2021 hadi 44,000 km mwaka 2024, ukiboresha usafiri wa bidhaa na watu vijijini.
14. Ongezeko la Malipo kwa Wazee Wastaafu
Kima cha chini cha malipo kwa wazee wastaafu kimeongezeka kutoka Tsh 100,000 hadi 150,000 kwa mwezi, hatua inayolinda heshima ya wazee waliolitumikia taifa.
15. Kuongeza Kima cha Chini cha Mshahara
Serikali imepandisha kima cha chini cha mshahara kutoka Tsh 370,000 hadi 500,000, ikiwalenga watumishi wa kipato cha chini ambao walikaa muda mrefu bila nyongeza.

16. Kuongeza Eneo la Umwagiliaji
Eneo la umwagiliaji limeongezeka kutoka hekta 540,000 hadi 980,000, likiwa sawa na takriban robo ya juhudi zote za miaka 60 zilizopita. Ongezeko hili linawaondoa wakulima kwenye utegemezi wa mvua zisizo na uhakika.
17. Kuongeza Mbolea ya Ruzuku
Serikali imeongeza mbolea ya ruzuku kutoka tani 600,000 mwaka 2021 hadi tani 1,200,000 mwaka 2024, ikilenga kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima wadogo.
18. Kuwapa Wachimbaji Wadogo Fursa
Serikali imebadili mfumo wa hati za madini ili wachimbaji wadogo wanufaike zaidi. Mchango wao kwenye mapato ya sekta ya madini umeongezeka kutoka 20% hadi 40% ndani ya miaka minne.
19. Mikopo kwa Wanafunzi wa Vyuo vya Kati
Kwa mara ya kwanza katika historia, wanafunzi wa vyuo vya kati wameanza kupata mikopo ya elimu, hatua kubwa kwa vijana wanaotoka familia zenye kipato cha chini.



20. Kuongeza Posho ya Kujikimu kwa Wanafunzi
Posho ya kila siku kwa wanafunzi wanaopata mikopo imeongezeka kutoka Tsh 8,500 hadi 10,000, ikilenga kuwasaidia watoto wa familia masikini kumudu maisha chuoni.
Hitimisho
Kwa muda wa miaka minne tu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha dira thabiti ya uongozi unaoelekeza nguvu kwa wanyonge kupitia elimu, afya, kilimo, ajira na miundombinu. Maamuzi haya 20 si takwimu pekee, bali ni ushahidi wa dhati kuwa maendeleo ya Tanzania yana mizizi katika usawa wa kijamii na uwezeshaji wa wananchi wa kipato cha chini.