Dkt. SAMIA NA MARAIS WENGINE WALIO MTANGULIA.

Tangu Tanganyika kupata Uhuru mwaka 1961, Tanzania imeongozwa na viongozi mahiri, kila mmoja akiwa na mtindo na falsafa yake ya uongozi. Kutoka kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi Rais Samia Suluhu Hassan, kila awamu imejenga msingi wa taifa kupitia maamuzi, sera, na ujasiri wa kisiasa. 

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na sauti za shaka kutoka baadhi ya watu wanaotilia shaka uamuzi au msimamo wa Rais Samia, mara nyingi wakisahau kuwa yale anayofanya ni mwendelezo wa mamlaka ya kawaida ya urais, kama walivyofanya waliomtangulia.

Urais wa Nyerere – Maamuzi Yasiyotetewa kwa Moyo Mwepesi

Mwalimu Nyerere alijulikana kwa uthubutu na maamuzi makubwa yasiyopingika kuanzia kuanzisha ujamaa inavyosemekana na mbinu na njia ambazo wengine wanazililia hadi leo, siasa za vyama vingi, na hata kujiuzulu mwenyewe mwaka 1985 ili kutoa nafasi kwa kizazi kipya. Alifanya maamuzi hayo kwa kuamini kuwa ni kwa maslahi ya taifa, bila kuruhusu hofu au shinikizo la kisiasa.

Uamuzi wake wa kuanzisha mashirika ya umma na kufuta kodi fulani ulipingwa, lakini ulikuwa sehemu ya mamlaka yake ya kikatiba.

Urais wa Mwinyi – Kufungua Milango ya Uchumi

Rais Ali Hassan Mwinyi, “Mzee wa Rukhsa,” alikumbwa na upinzani alipofungua uchumi na kuruhusu biashara binafsi. Wengi walimkosoa wakisema anavunja misingi ya ujamaa, lakini historia ilionyesha alifanya kile kilichohitajika wakati huo. Hakuwa dhaifu alikuwa na mabadiliko yenye maono.

Mkapa – Nidhamu, Uwazi na Ubinafsishaji

Rais Benjamin Mkapa alileta ubinafsishaji wa mashirika ya umma, kitu ambacho wengine wamemlaani hadi leo, na ni sera iliyokuwa ngumu kisiasa. Lakini Alikosoa ufisadi, akaanzisha misingi ya utawala bora, na akasimamia uwajibikaji. Wapo waliomwona kama mkali na mgumu, lakini maamuzi yake yalibadilisha taswira ya uchumi wa Tanzania.

Kikwete – Diplomasia na Uwekezaji

Jakaya Mrisho Kikwete alijulikana kwa ucheshi, diplomasia, na kufungua taifa kimataifa. Hata hivyo na yeye pamoja na ucheshi wake. Alipitia mengi yaliyosemwa na kushutumiwa. Uwekezaji na miradi mikubwa ilianza enzi yake, akitumia mamlaka ya urais kuvutia wawekezaji na kukuza sekta ya miundombinu. Wapo waliomuita “mpole kupita kiasi,” lakini rekodi za maendeleo zilizungumza.

Magufuli – Nidhamu, Utekelezaji, na Msisitizo wa Uwajibikaji

Hayati John Pombe Magufuli alikuwa mfano wa uthubutu. Alisimamia nidhamu ya kazi, akaongeza mapato ya serikali, na kubana matumizi. Wapo waliomwona kuwa mkali mno, na waliokua karibu yake tu ndio walionufaika, wengine kufika mbali hadi kusema ni mkabila na anachukia walio nacho.

Hata hivyo hatuwezi kubisha kuwa alitumia mamlaka yake ya kikatiba kwa njia aliyoamini inalinda taifa. Hakupenda kuhojiwa, lakini historia itamkumbuka kwa ujasiri.

Samia Suluhu Hassan – Uongozi thabiti, Kusikiliza na Kujenga Maridhiano

Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeleta sura mpya katika siasa na maendeleo ya Tanzania. Tofauti na viongozi waliomtangulia, Samia alichagua njia ya hekima, maridhiano na diplomasia badala ya mabavu na migawanyiko.

\Amejenga upya uhusiano wa kimataifa, kuvutia wawekezaji, na kuimarisha sekta za kimkakati kama kilimo, nishati, na teknolojia ya kidigitali.

Kupitia miradi kama Royal Tour na BBT – Building a Better Tomorrow, amebadilisha taswira ya Tanzania kuwa taifa la fursa na ubunifu. Samia anaongoza kwa ustahimilivu akiweka matokeo mbele ya makelele  na kwa kufanya hivyo, anathibitisha kuwa urais siyo sauti kali, bali uwezo wa kuongoza kwa akili, uadilifu na matokeo.

Rais Samia Suluhu Hassan, kiongozi wa kwanza mwanamke nchini, amechukua hatua tofauti, si kwa udhaifu, bali kwa uelewa wa nyakati. Ameweka msisitizo kwenye diplomasia, maridhiano ya kisiasa, mageuzi ya sekta ya kilimo, uwekezaji wa kimkakati, na ushirikishwaji wa vijana na wanawake katika maendeleo.

Ametambua kuwa taifa linaweza kujengwa kwa ushirikiano, sio migawanyiko. Na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kila Rais ana mamlaka kamili ya kuteua, kubadilisha, na kusimamia serikali kulingana na maono yake ya kitaifa.

Anatekeleza Mamlaka Kikatiba, Kila Rais ana mtindo wake wa kutumia madaraka, na yeye anaendelea kwa misingi hiyo hiyo. Anajenga Tanzania ya Kisasa: Kupitia mageuzi ya kidigitali, uwekezaji wa kijinsia, na diplomasia ya kiuchumi.

Anapunguza Migawanyiko: Wakati wengine waliongoza kwa mkono wa chuma, yeye anajenga maridhiano bila kuacha misimamo.

Anatambua Nguvu ya Ushawishi: Dunia ya leo inataka ushawishi, si mabavu. 

Historia inatufundisha kuwa kila Rais wa Tanzania amekuwa na mtindo wake lakini wote wamekuwa ndani ya mipaka ya mamlaka yao ya kikatiba. Samia Suluhu Hassan anatembea katika nyayo hizo hizo.

Tofauti yake ni namna anavyotumia hekima, ushirikiano, na uelewa wa dunia ya sasa katika kujenga taifa lenye heshima, amani, na maendeleo. Yeye ni kiongozi wa nyakati mpya,  mwenye hekima ya kisasa, na ujasiri wa mwanamke anayeamini kwamba Tanzania inaweza kuongozwa kwa akili, si kwa hofu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *