Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuimarisha uhusiano wake wa muda mrefu na Vatican (Holy See) baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (MB), kupokelewa katika mazungumzo maalum na Baba Mtakatifu Papa Leo XIV mjini Vatican.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Kombo amewasilisha salamu za dhati na ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kueleza shukrani za Serikali kwa msisitizo wa Papa katika masuala ya amani, mazungumzo na utu wa binadamu misingi ambayo Tanzania inaiona kuwa nguzo muhimu za utulivu, haki na mshikamano wa kimataifa.
Waziri Kombo amebainisha kuwa kwa miaka mingi Tanzania imeimarika kupitia ushirikiano wake na Vatican, ushirikiano unaojengwa juu ya heshima, huduma kwa jamii na imani ya pamoja katika utu wa binadamu. Akibainisha kuwa mchango wa Kanisa Katoliki unaonekana wazi katika maisha ya Watanzania kupitia sekta za elimu, afya na huduma kwa makundi yaliyo pembezoni, sambamba na juhudi za maendeleo ya Taifa.

Serikali imetoa shukrani kwa taasisi za Kikatoliki zinazoendelea kuunga mkono maendeleo ya elimu, afya na jamii, pamoja na fursa zinazotolewa kwa wanafunzi wa Kitanzania kusoma katika taasisi za Kipapa. Waziri pia ameeleza fursa hizo huchangia kujenga ujuzi, maadili na kuimarisha mahusiano ya kudumu baina ya watu.
Mhe. Kombo pia amesisitiza kutambua mchango muhimu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) katika maisha ya kijamii na kiraia, na kuthibitisha dhamira ya Serikali kuendeleza ushirikiano wa wazi, wa heshima na wa kujenga na Kanisa katika ngazi zote kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Akizungumzia matukio ya vurugu yaliyotokea katika baadhi ya maeneo baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025, Waziri ameeleza dhamira ya Serikali kurejesha utulivu na hali ya kawaida, akibainisha kuwa Rais Samia ameielekeza Serikali kujenga upya imani na umoja wa kitaifa, ikiwemo kuanzishwa kwa mchakato huru wa mapitio unaoongozwa na Jaji Mstaafu ili kubaini ukweli, kujifunza na kuzuia kurejea kwa matukio hayo.
Serikali imesisitiza dhamira ya Rais ya kuendeleza mazungumzo jumuishi na vyama vya siasa, wazee, vijana, viongozi wa dini na asasi za kiraia, kwa kuongozwa na falsafa ya 4R: Maridhiano (Reconciliation), Ustahimilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms) na Kujenga Upya (Rebuilding). Katika muktadha huo, Waziri amemuomba Baba Mtakatifu kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania amani, umoja na mafanikio ya mchakato huo wa kitaifa.
Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Papa Leo XIV amekaribisha ombi hilo na kuahidi kuliombea Taifa la Tanzania. Akikumbuka kwa dhati miaka ya nyuma kwamba aliwahi kukaa nchini Tanzania, akitaja uzoefu wake wa kichungaji katika miji ya Songea, Morogoro, Arusha na Dar es Salaam, uliomjengea uhusiano wa kudumu na Watanzania.

Mbali na mazungumzo na Papa, Mhe. Kombo na ujumbe wake, viongozi hawa walifanya mazungumzo rasmi na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican anayesimamia Mahusiano na Nchi na Mashirika ya Kimataifa, kwa lengo la kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimfumo kati ya Tanzania na Vatican.
Katika mazungumzo hayo, Tanzania imepeleka ombi kwa Vatican la kuanzishwa kwa uwakilishi wa kidiplomasia wa kudumu wa Tanzania mjini Vatican, hatua itakayosaidia kuimarisha ushirikiano na mawasiliano ya mara kwa mara. Kwa sasa, Tanzania inawakilishwa na Balozi asiye mkazi, Mhe. Hassan Iddi Mwamweta, mwenye makazi yake Berlin.
Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (MB), ukiwajumuisha Mhe. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Nchi; Balozi Hassan Iddi Mwamweta; na Balozi Noel E. Kaganda, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Serikali imeeleza kuwa ziara hiyo inaakisi mwelekeo wa diplomasia ya Tanzania kwa mwaka 2026 kama ilivyoelezwa na Rais Samia juu ya sera ya “kutofungamana lakini kushirikiana kwa upana” (non-aligned but multi-engaged), inayolenga ushirikiano wa dhati na washirika wote kwa maslahi ya umoja wa kitaifa na ustawi wa pamoja.