**Jaji Mutungi: Lissu Hawezi Kuzuia Uchaguzi Mkuu** **Jaji Mutungi: Lissu Hawezi Kuzuia Uchaguzi Mkuu**

JAJI MUTUNGI: LISSU HAEZI KUZUIA UCHAGUZI MKUU

Msajili afunguka kuhusu Lissu

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amesema kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, hawezi kuzuia uchaguzi mkuu kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Jaji Mutungi ameeleza kuwa kauli za Lissu ni propaganda za kisiasa zinazofanywa na baadhi ya wanasiasa, na hivyo wananchi wanapaswa kuzipuuza. Alitoa kauli hiyo jana alipoulizwa kuhusu hatua zinazochukuliwa na ofisi yake dhidi ya matamshi ya vitisho yanayotolewa na Lissu, ambayo yanaashiria uwezekano wa kuvuruga amani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Lissu, akizungumza hivi karibuni na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alisisitiza kuwa chama chake hakitashiriki uchaguzi endapo sheria na mfumo wa uchaguzi havitafanyiwa mabadiliko.

Lissu alieleza kuwa anazidi kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii ili kuhamasisha msimamo wa CHADEMA kuhusu kaulimbiu yao ya No Reforms, No Elections (Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi).

Jaji Mutungi, akijibu kauli za Lissu, alisema:

“Lissu anajua kuwa kuzuia uchaguzi haiwezekani kisheria. Anachofanya ni propaganda tu za kisiasa, na mimi nashauri apuuzwe kwa sababu hana uwezo wa kuzuia uchaguzi.”

Ripoti za Tume na Msimamo wa CHADEMA

Katika mkutano wake na wahariri, Lissu alifichua kuwa msimamo wa CHADEMA wa kutoshiriki uchaguzi bila mabadiliko ulitokana na ripoti za tume tatu zilizoundwa na marais wa awamu tatu tofauti. Ripoti hizo zilichangia Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CHADEMA, chini ya uongozi wa Freeman Mbowe, kupitisha azimio la No Reforms, No Elections.

Lissu alisema kuwa utekelezaji wa azimio hilo umeanza kwa kukutana na viongozi wa makundi yenye ushawishi mkubwa nchini, wakiwemo wazee, viongozi wa dini, asasi za kiraia, na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Akizungumzia mfumo wa uchaguzi, Lissu alisema kuwa ripoti za tume mbalimbali, zikiwemo zile zilizoongozwa na majaji Francis Nyalali, Robert Kisanga, na Joseph Warioba, zinaonyesha kuwa mfumo wa uchaguzi nchini hautoi haki kwa vyama vya upinzani bali unanufaisha chama tawala, CCM.

Hoja za Lissu kuhusu Mfumo wa Uchaguzi

Lissu alieleza kuwa mfumo wa uchaguzi nchini unakandamiza upinzani na kutoa ushahidi wa uchaguzi wa 2019, 2020, na 2024. Pia, alidai kuwa mfumo wa kugawa majimbo haufuati usawa wa uwakilishi wa wananchi. Alitoa mfano wa Zanzibar yenye majimbo 50, wakati Dar es Salaam yenye idadi kubwa zaidi ya watu ina majimbo 10 pekee.

“Mfumo huu wa mgawanyo wa majimbo umevurugwa na hauna uwiano wa haki. Majimbo mengine yanaanzishwa kwa lengo la kuwasaidia baadhi ya watu kurudi bungeni,” alisema Lissu.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi, alisisitiza kuwa uchaguzi mkuu utafanyika kama ilivyopangwa, na kauli za Lissu hazipaswi kuwatia hofu wananchi.

Kwa upande wake, Lissu ameendelea kusisitiza kuwa hakuna uchaguzi utakaofanyika bila mabadiliko ya msingi katika mfumo wa uchaguzi, akisema kuwa CHADEMA itaendelea kushinikiza mabadiliko hayo kwa njia za kidemokrasia.

Credit> Raia mwema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *