Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Rais Samia Suluhu Hassan, wote tumemshuhudia kama kiongozi anayejali maridhiano, amani, na maendeleo ya Taifa. Kupitia falsafa yake ya 4R —Kurekebisha, Kujenga, Kurejesha, na Kuboresha, ambayo imefanikisha kuirejesha Tanzania kwenye mstari wa mazungumzo ya kitaifa, ili kuondosha siasa za uhasama na mifarakano ili kuchochea ushirikiano baina ya vyama vya siasa nchini.
Hata hivyo, juhudi za Rais Samia zinaonekana kukubwa na changamoto ya ukuta wa baadhi ya wasaidizi wake ambao, badala ya kuunga mkono malengo yake, wamekuwa kikwazo kikubwa. Vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kama vile utekaji, vitendo vya kinyama na uvunjifu wa sheria vinaendelea kwa kasi, hali inayokinzana kabisa na dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha utawala wa sheria na haki.
Utekelezaji wa Maridhiano na Amani
Rais Samia, akiwa mtu mwenye kuamini sana katika nguvu ya sheria na maridhiano, amechukua hatua kadhaa kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi ya amani. Alipoingia madarakani, alianzisha juhudi za kufungua milango ya mazungumzo kati ya pande mbalimbali za kisiasa nchini, huku akijitahidi kurejesha imani ya umma kwa serikali.
Tumeshuhudia jinsi alivyofanikisha majadiliano na upinzani, jambo lililokuwa nadra katika miaka iliyopita. Amewaita wapinzani na wadau mbalimbali wa kijamii kushirikiana kwa maslahi ya taifa, huku akisisitiza umuhimu wa haki na utawala bora.
Lakini changamoto inaonekana pale ambapo baadhi ya wasaidizi wake wanshindwa kumuelewa au kudharau maono yake wakitumia nafasi na madaraka waliyonayo kuenenda kinyume kwa maslahi yao.
Vitendo vya utekaji na uvunjaji wa haki za binadamu vinaendelea, na hili linaibua swali la msingi: Je, Rais Samia ataweza vipi kufanikisha azma yake ikiwa baadhi ya viongozi wanaomsaidia wanapita mlango wa nyuma na kufanya mambo yao binafsi tofauti na maono yake?
Tunatambua na kuamini kuwa Rais Samia, ni kiongozi wa kipekee ambaye anajua nguvu ya sheria na umuhimu wa kuhakikisha haki inatendeka kwa wote. Hii inajidhihirisha Katika hotuba na matamko yake, mara nyingi ameonesha kutokubaliana na vitendo vya uvunjaji wa haki na kuhimiza utawala wa sheria.
Lakini pamoja na maagizo na maelekezo yake, inasikitisha kuona kuwa baadhi ya watendaji na wasaidizi wake wanashindwa kufuata falsafa hiyo ya haki na amani, si ajabu kuona kila mara tukishuhudia teuzi na tenguzi kutokana na baadhi ya watendaji wa serikali kushindwa kuenenda sawa sawa na falsafa ya Mhe Rais. Ni ni kwa sababu , badala ya kuwa nguzo ya kusaidia ajenda yake, wamekuwa kikwazo, wakivuruga kazi nzuri anayojaribu kuifanya.
Ni wazi kuwa si rahisi kwa kiongozi yeyote kufanya kila kitu peke yake. Taifa kubwa kama Tanzania linahitaji timu ya watendaji waaminifu, wazalendo na wachapa kazi wanaounga mkono falsafa ya kiongozi wao pasipo kuingiza mambo yao binafsi yenye kuwanufaisha wao wenyewe.
Kwa bahati mbaya, baadhi ya viongozi wa serikali wanashindwa kuendana na falsafa ya Rais Samia ya amani, maridhiano, na haki. Wameonekana kufumbia macho mambo mabaya ikiwamo suala la utekaji na mwendelezo wa matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu yanayoendelea, hali inayotishia kuharibu sifa nzuri ambayo Rais Samia ameijenga tangu alipoingia madarakani.
Vitendo vya utekaji vinavyoripotiwa, ukandamizaji wa baadhi ya haki za raia, na maamuzi yasiyoendana na kauli mbiu ya maridhiano ni ishara wazi kuwa kuna watendaji ambao wameshindwa kutekeleza wajibu wao. Wameshindwa kumuunga mkono Rais Samia, ambaye kila siku anajitahidi kujenga nchi inayoheshimu haki na utu wa kila raia. Rais amekabidhiwa jukumu zito la kuiunganisha Tanzania.
Je, Rais Anaweza Kufanya Yote Peke Yake?
Swali hili tunapaswa kujiuliza sisi wote kama taifa: Je, ni haki kumtegemea Rais Samia pekee kutatua matatizo yote? Rais ameweka misingi imara ya maridhiano na haki, lakini anahitaji msaada wa wasaidizi wake ili kufanikisha malengo haya.
Kama viongozi hawatatekeleza maelekezo yake, ni wazi kuwa kazi hiyo itakuwa ngumu mno. Ni jukumu la kila kiongozi, kutoka ngazi ya chini hadi juu, kuhakikisha kuwa wanafuata falsafa ya Rais na kuitekeleza kwa vitendo.
Kwa upande wake, Rais Samia tumeona akifanya kazi kubwa kujenga imani ya Watanzania kwa serikali. Ameimarisha mahusiano ya kimataifa, ametoa fursa kwa vijana, na kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa nchi yenye amani na ushirikiano. Ameweka wazi kuwa Tanzania ni nchi ya haki, na hakuna aliye juu ya sheria tofauti na miaka kadhaa ya nyuma.
Hitimisho
Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kuwa kiongozi na mbeba maono makubwa ya watanzania. Amejidhihirisha kuwa kiongozi anayejali haki, amani, na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Ili kuhakikisha kuwa Tanzania inasonga mbele kwa kasi, ni lazima watendaji wa serikali wawe sehemu ya suluhisho, si sehemu ya tatizo. Wasaidizi wa Rais lazima waelewe kuwa mafanikio ya Tanzania yanategemea sana ushirikiano na utekelezaji wa falsafa ya maridhiano na haki inayohubiriwa na Rais Samia.
Pamoja na hayo, Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha anakuwa balozi wa amani nchini, na kupinga kwa nguvu zote matukio ya uvunjifu amani ambayo tumeridhi toka kwa wazee wetu kwa manufaa ya taifa zima. Wasaidizi na watumishi wa vyombo vya usalama lazima wendelee, kumuunga mkono Mhe Rais kwa vitendo na kwa mujibu wa misingi ya haki ili Tanzania iendelee kuwa nchi ya amani, haki, na maendeleo endelevu.