Mapambano Yasiyoonekana Kwa Karibu na Wengi
Na Mwandishi
Hivi sasa nchi ya Tanzania tunakabiliwa na presha kubwa ya kimataifa kuliko inavyoonekana. Mivutano hii ya kisiasa mitandaoni inayoshuhudiwa leo si jambo jipya wala la ghafla. Kamahufahamu chanzo chake ni uamuzi uliofanywa mwaka 2017 uamuzi uliogusa maslahi ya mabwana wakubwa wa rasilimali duniani.
Sheria Zilizotikisa Mfumo wa Uchumi wa watu fulani.
Mwaka huo, Bunge la Tanzania lilipitisha sheria mbili muhimu:
- Sheria ya Umiliki wa Kudumu wa Rasilimali za Taifa
- Sheria ya Mapitio Upya na Majadiliano ya Mikataba ya Rasilimali
Kupitia sheria hizo, Tanzania ilitangaza ajenda mpya: inayofahamika kama “Rasilimali zetu, masharti yetu, maamuzi yetu.”
Kauli hiyo ilitosha kuibua taharuki kwa miji mikubwa ya fedha duniani London, Washington, na kwingineko. Kwa mara ya kwanza, Tanzania ikasema hapana kwa mfumo ambao kwa miongo mingi umeruhusu faida kubwa kurudi nje ya nchi kuliko inavyonufaisha Watanzania.
Magufuli na “Vita ya Kiuchumi”
Mwendazake Rais Dkt. John Magufuli hakuficha alichokiona. Aliita hali hiyo vita ya kiuchumi na hakuwa na masihala kabisa
Katika vita hii:
- Tanzania ililinda mikataba ya madini dhidi ya mashinikizo ya kimataifa
- Kampuni kubwa za uchimbaji zilianza kupoteza nafasi
- Sauti za kukosoa demokrasia na uhuru wa habari zikaongezeka ghafla
Baadhi ya hofu ni kweli zilikuwa na uhalisia. Lakini sehemu kubwa ya kelele zilitengenezwa kwa makusudi kutengeneza shinikizo la kurejesha ushawishi wa zamani.
Mabadiliko Ya Uongozi mwaka 2021, Je Mwelekeo Ulibadilika?
Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani, diplomasia ikawa agenda yake baada ya kukutana na Nchi za Magharibi zikajiliwaza kuwa hatimaye, Tanzania imelegeza msimamo. Lakini kilichokuwa kinaendelea ndani ya sera za uchumi Hakikuwahi kubadilika.
Serikali iliendelea kuwekeza kwenye miradi ambayo ilizidi kuweka wasiwasi hususani kimataifa mfano miradi ya,
- Mkuju Uranium — mradi unaogusa usalama wa kimataifa kwa sababu uranium ni nyenzo ya nyuklia. Na Tanzania imechagua kushirikiana na Russia (Rosatom).
- Lindi LNG — Gesi yenye thamani kwa muongo ujao, ambapo China na nchi za Ghuba zimekuwa na nguvu kubwa kuliko kampuni za Magharibi katika madili haya.
Kwa mataifa yenye maslahi makubwa, ujumbe ukawa dhahiri Tanzania bado haijarudi kwenye enzi zile za masharti.
Vita Inageukia Kidijitali
Tunapaswa kutambua kuwa Karne hii si ya mapanga na vifaru tena. Ni karne ya propaganda, taarifa, na ajenda zinazoandaliwa kwa ustadi kupitia:
- Mitandao ya kijamii
- Influencers na bots
- Makundi ya siasa yaliyogawanyika
- Vijana wenye matarajio makubwa na hali ngumu ya kiuchumi
Kuanzia 2023, Tanzania tumeanza kujikuta katikati ya mlipuko wa ajenda za mtandaoni nyingi zikiwa na ushawishi wa kimataifa.
Utakumbuka Julai 2025, Serikali ilitoa Tamko la Mkuju, ishara wazi ya msimamo wa kitaifa, utakumbuka bandari na mengine mengi yote yalizidisha kelele kutoka mataifa ya magharibi bila kusahau bomba la mafuta ambalo lilianza kutengenezwa figisu za mambo ya kimazingira.
Haya yote si ajali. Ni matokeo ya shinikizo la miaka nane dhidi ya taifa lililochagua namna ya kulinda rasilimali zake.
Tunapaswa kufahamu kuwa haya tunayoyaona sio machafuko halisi ya kitanzania, ni mbinu za watu katika maslahi yao.
Tanzania leo iko katikati ya mapambano makubwa yenye nguvu duniani:
- Mashariki dhidi ya Magharibi
- Madini na gesi dhidi ya siasa
- Uhuru wa kiuchumi dhidi ya urithi wa enzi za kikoloni
Hivyo, mijadala inayopamba moto mitandaoni usidhani yanalenga kuwasilisha sauti ya wananchi peke yao bali pia ni milio ya vita ya kijasusi ya kibiashara inayopiganwa kwa mbinu mpya.
Hatima ya nchi hii haitategemea nani anashinda mabishano tunayoyaona mitandaoni, bali iwapo tutalinda maslahi ya taifa bila kuvunjika kwa propaganda za nje. Kwa sababu mwisho wa yote Tanzania ndiyo itakayobeba ushindi ama majeraha ya mchezo huu.