TANZANIA YAENDELEA KUWA IMARA NA RAFIKI KWA WAWEKEZAJI TANZANIA YAENDELEA KUWA IMARA NA RAFIKI KWA WAWEKEZAJI

TANZANIA YAENDELEA KUWA IMARA NA RAFIKI KWA WAWEKEZAJI

Na Alex Malanga

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa hakikisho jipya kwa jumuiya ya wawekezaji wa kimataifa kuwa Tanzania imeendelea kuwa nchi tulivu, thabiti kwa ajili ya uwekezaji. Kauli hiyo ameitoa katika mazungumzo yake na Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Biashara na Uwekezaji la Jumuiya ya Madola (CWEIC), Lord Hugo Swire KCMG, yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Mazungumzo kati ya viongozi hao yalilenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji yatakayochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Katika maelezo yake, Rais Samia ameelezea kuwa mkakati wa serikali ni kuvutia uwekezaji wa muda mrefu katika sekta muhimu ikiwemo viwanda, kilimo-biashara, nishati na miundombinu ya usafirishaji. Akisisitiza kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wawekezaji wanaoonesha nia ya dhati ya kuwekeza nchini.

Katika tathmini ya safari ya zaidi ya miaka sitini ya Tanzania tangu kupata uhuru, Rais Samia ameeleza kuwa taifa limeendelea kujenga mazingira rafiki, yenye utulivu na yanayohamasisha ukuaji wa biashara na uwekezaji.

Sehemu muhimu ya mazungumzo hayo pia ilihusu kuongeza imani kwa wawekezaji kufuatia matukio ya Oktoba 29, 2025. Rais Samia amebainisha kuwa mifumo ya utawala nchini iko imara na ina uwezo wa kusimamia masuala ya ndani bila kuyumbishwa na changamoto yoyote. Aidha, amewahakikishia wawekezaji kuwa serikali imechukua hatua thabiti kulinda ustahimilivu wa taifa na kulinda rasilimali zote za uwekezaji zilizopo nchini.

Katika hatua ya kuimarisha zaidi msingi wa uwazi na uwajibikaji, Rais Samia amefichua kuwa tayari Tanzania imeanza hatua za awali za kupitia Katiba. Mchakato huo, unalenga kuboresha utendaji wa taasisi, kuimarisha uwajibikaji na kurahisisha shughuli za kufanya biashara maeneo muhimu kwa kuongeza imani ya wawekezaji.

Kwa upande wake, Lord Swire amepongeza hatua hizo na kubainisha kuwa CWEIC inaiona Tanzania kama kitovu muhimu cha ukuaji katika Jumuiya ya Madola. Akionesha utayari wa Baraza hilo kuongeza ushirikiano, kuratibu misafara ya uwekezaji, na kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na masoko ya Jumuiya ya Madola.

Mazungumzo hayo yamehitimishwa kwa pande zote mbili kuonesha dhamira ya kuharakisha programu zinazolenga kukuza biashara, mtiririko wa uwekezaji na fursa za ajira kwa Watanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *