Ripoti ya Hali ya Demokrasia Duniani ya mwaka 2023, iliyotolewa na Economist Intelligence Unit (EIU) kupitia Democracy Index, inaitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa masuala ya demokrasia katika Afrika Mashariki. Tanzania imepewa nafasi ya 12 kikanda na ya 86 duniani, ikifuatiwa na Kenya katika nafasi ya 14 kikanda na 92 duniani, huku Uganda ikishika nafasi ya 16 kikanda na 99 duniani.
Vigezo vilivyotumika kutoa alama hizi ni pamoja na mchakato wa uchaguzi, mfumo wa vyama vingi, utendaji wa serikali, ushiriki wa wananchi katika siasa, utamaduni wa kisiasa, na uhuru wa raia.
Kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania imeendelea kuimarika katika vigezo hivi, kwa kufuata misingi ya falsafa yake ya “4R”: Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reform (Mageuzi), na Rebuilding (Ujenzi Mpya).
Falsafa hii imekuwa msingi wa uongozi wa Rais Samia, ambao umejikita katika kuimarisha amani, utawala bora, na demokrasia nchini. Kupitia utekelezaji wa falsafa hii, serikali imekuwa ikijenga mazingira bora ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii, na hivyo kuchochea maendeleo shirikishi na endelevu kwa wananchi wote.
Hatua Kubwa za Kisheria na Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi.
Katika Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mwaka 2024/25, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alieleza kuwa, katika juhudi za kuhakikisha demokrasia inaimarika, Bunge lilitunga Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani. Marekebisho haya yalihusisha pia Sheria za Vyama vya Siasa, hatua ambayo inalenga kuhakikisha usimamizi wa uchaguzi unakuwa bora zaidi.
Sheria hizi zinaweka mazingira ya uchaguzi uliohuru na wa haki, unaoendeshwa na kusimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Serikali pia imeendelea kuhakikisha vyama vya siasa vinapata fursa sawa katika uendeshaji wa shughuli zao. Mwaka 2023/2024, serikali ilitoa ruzuku ya Shilingi bilioni 11.7 kwa vyama vya siasa vinavyostahili kupata ruzuku hiyo, hatua ambayo imesaidia kuimarisha demokrasia nchini.
Maoni ya Wadau wa Siasa Kuhusu Uimarishaji wa Demokrasia.
Wadau wa masuala ya siasa na wanasiasa mbalimbali wanaamini kuwa demokrasia ni msingi wa kuleta maendeleo shirikishi. Dk. Paul Loisulie, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), anasema falsafa ya 4R imechangia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini. Kwa sasa, vyama vya siasa vina uhuru wa kufanya maandamano na mikutano ya ndani, jambo ambalo lilikuwa changamoto miaka ya nyuma.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, anaeleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika demokrasia chini ya uongozi wa Rais Samia. Anaongeza kuwa, ukuaji wa demokrasia unahitaji kuendana na uwepo wa katiba mpya itakayoweka misingi imara ya sheria zinazohusu masuala ya demokrasia.
Magdalena Sakaya, mwanasiasa maarufu, anasema Tanzania imepiga hatua kubwa kidemokrasia ukilinganisha na miaka ya nyuma, na kwamba juhudi zaidi zinahitajika ili kuimarisha demokrasia bora katika Afrika. Dennis Konga, Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, anasema demokrasia inahusisha ushiriki wa watu katika masuala mbalimbali, ikiwemo kupiga kura na uchaguzi, na hivyo kuchangia maendeleo ya wananchi.
Changamoto na Mapendekezo ya Kuimarisha Demokrasia.
Licha ya mafanikio haya, bado kuna changamoto zinazohusiana na matumizi mabaya ya demokrasia na baadhi ya wanasiasa. Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Mbeya (CUoM), Samson Mwigamba, anaeleza kuwa demokrasia imekua nchini, lakini anasisitiza umuhimu wa kukabiliana na wanasiasa wanaotumia vibaya uhuru huu kwa kukashifiana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa habari ,Uenezi, Mahusiano na Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa, anasema chama chake kimefarijika na falsafa ya 4R ya Rais Samia, ingawa wanakabiliwa na changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa falsafa hiyo. Katibu mstaafu wa Bunge, George Mlawa, anasisitiza kuwa kukua kwa demokrasia nchini kunapaswa kumpa kila mtu uhuru wa kugombea nafasi za uongozi, hata bila kuwa na chama cha siasa.
Kwa ujumla, maendeleo ya demokrasia nchini Tanzania ni ushuhuda wa juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine kuhakikisha kuwa nchi inasonga mbele kwa kuimarisha misingi ya utawala bora, amani, na maendeleo shirikishi kwa wananchi wote.
Credit> Habari Leo.