Matukio yaliyotokea nchini hivi karibuni ni ukweli usiopingika kuwa hayakuwa maandamano kama walivyodai hapo mwanzoni bali yalikuwa ni vurugu na uharibifu mkubwa ulioacha alama chungu kwa Taifa. Mali za umma na binafsi zenye thamani ya mabilioni ya shilingi zilichomwa moto, kuharibiwa na kuporwa hali iliyoathiri kwa kiasi kikubwa uchumi, shughuli za wananchi na taswira ya nchi.

Pamoja na ukubwa wa uharibifu huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kusimama na watanzania, akiamini kuwa wapo waliofanya vurugu lakini pia wapo waliokamatwa kwa kufanya vurugu za kufuata mkumbo, ndio maana akatangaza msamaha kwa watu hao sambamba na kuachiwa huru baada ya jeshi la polisi kujiridhisha.
Katika siasa tunaweza kusema hii ni hatua ya ukomavu na busara, yenye kuonesha dhamira ya Serikali kutanguliza maridhiano, upole na kuponya Taifa badala ya kuendelea kugawanyika.
ATHARI ZA KIUCHUMI: UCHUNGU WA UHARIBIFU WA MIUNDOMBINU YA MWENDOKASI
Mojawapo ya maeneo yaliyoathirika sana ni miundombinu ya Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi (BRT) jijini Dar es Salaam. Sio kwa bahati mbaya kwani toka siku ya kwanza wanaharakati wa mtandaoni walikuwa wakitoa maagizo kwa waandamanaji kuchoma, kuharibu maeneo mbali mbali ambayo ni msaada kwa wananchi wakifahamu fika wapo nje ya nchi na hawatumii miradi hii ikiwemo Mradi wa Mwendokasi uliogharimu serikali mamilioni ya fedha,
Fedha za wananchi wenyewe, mradi ukilenga kuboresha usafiri wa umma, kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi kwa wafanyakazi na wafanyabiashara. Lakini sehemu kubwa ya miundombinu hiyo imeharibiwa, vituo vimechomwa moto, na hadi sasa baadhi havijarejea katika hali ya kawaida, hizi ni gharama nyingine ambazo kama taifa tutapaswa kuzitafuta na kuzitumia pengine kusubirisha miradi mingine ya maendeleo ili tuweze kukabiliana na hasara hii.
Uharibifu huu haukuathiri tu barabara na majengo, bali umeathiri maisha ya maelfu ya Watanzania wanaotegemea usafiri huo kila siku kwenda kazini, kwenye biashara na mahitaji ya msingi. Umeathiri mapato ya Taifa, kuongezeka kwa gharama za matengenezo, na kuchelewesha maendeleo yaliyokuwa yakitegemewa.

TUKUBALI UKWELI: TULIUMIA, NA TUNAPASWA KUJIFUNZA
Baada ya matukio mengi yaliyoacha majonzi kwa watanzania, ni kweli Kumekuwa na mkanganyiko wa taarifa kuhusu idadi ya vifo na majeruhi. Idadi ambayo haijatajwa na chombo chochote lakini wanaharakati hao hao wamekuwa wakitoa taarifa za mauwaji tena kwa wingi, jambo linaloshangaza kuwa kukuza namba hizo ni kufurahia wingi wa vifo?
Inawezekana si kweli ila ni sehemu ya matokeo ya uchafuzi wao ambayo yanaweza kuwapatia fedha nzuri kutoka kwa mabeberu wanaodhamini vita na machafuzi haya, wewe unalia yeye anapata ndio maisha yalivyo.
Ndio tuna wingi wa Taarifa mbalimbali bado hazijathibitishwa rasmi, lakini ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya watu walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Huu ni ukweli ambao Rais aliutaja hadharani katika hotuba yake bungeni, na yeye mwenyewe akasisitiza utulivu wakati Serikali inasubiri ripoti kamili ya Tume ya Uchunguzi.
Ni lazima tujiulize kama Watanzania:
Je, hii ndiyo hali tunayotaka?
Je, tuko tayari kuona amani yetu ikiyeyuka kwa matendo ya hasira na ushawishi wa watu ambao hawatutakii mema?
Wewe wakati unatafuta pesa ya kula na familia yako, umewahi kujiuliza wanaharakati wanaotoa maneno na matamshi kukutaka uingie barabarani wanaishi vipi huko walipo? Umewahi kujua kazi rasmi wanazofanya kuingiza kipato? Au wanaishi pasipo matumizi? Ama wanakupenda sana wewe na hivyo wamekubali kutoajiriwa ama kujiajiri ili wakae mtandaoni kuchapisha mambo ya kisiasa? Akili mtu wangu.
Kila mmoja aliona siku hizo za giza zilivyokuwa, Watanzania wengi walitamani siku iishe na hali itengemae. Tulitamani kurudi kazini, sokoni, mashambani, mtaani kwenye maisha ya kawaida ambayo ndiyo msingi wa kuishi kwetu. Maana kwa wengi wetu, kazi ndiyo maisha, na bila ya amani hakuna kazi, hakuna biashara, hakuna riziki.

TUCHAGUE HOJA BADALA YA VURUGU
Hakuna taifa duniani linalojenga mustakabali wake kwa chuki, ghadhabu na ghasia. Na kitu kimoja nimegundua ni kuwa nchi inayopatikana kwa kumwaga damu siku zote ata uje uongozi gani, uongozi utaendelea kutolewa kwa kumwaga damu, hii huwa inajirudia mara kwa mara kwaio usidhani kuwa kuna haki inayopatikana kwa kuharibu mali, kwa kuchoma majengo, kwa kuumiza watu. Ukianza kwa nguvu, utapata jibu la nguvu. Ndivyo ilivyo dunia nzima.
Haki hupatikana kwa kutumia hoja, majukwaa halali, mifumo ya kisheria na mijadala yenye heshima. Pale tunapokosewa, tunapaswa kuongea, lakini kuongea kwa amani, kwa hekima na kwa upendo wa Taifa letu.
TUREJEE KATIKA TANZANIA TUNAYOITAMBUA
Tanzania imejengwa kwenye misingi ya amani, umoja na utu. Ndiyo urithi wetu toka tumezaliwa. Ndiyo fahari yetu. Ndiyo nguvu yetu. Tukiruhusu hasira zitutangulie, tutaipoteza nchi ambayo wazee wetu waliilinda kwa gharama kubwa.
Tukubali yaliyotokea, tujifunze, tusameheane na tuanze upya.