UCHANGANUZI WA HOTUBA YA RAIS SAMIA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA JESHI LA POLISI TANZANIA.

Katika maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa hotuba yake ambayo bila shaka ilikuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na kundi kubwa la watanzania, kutokana kutokana na kushamiri kwa habari mbali mbali mtandaoni na katika vyombo vya habari  juu ya matendo ya kikatili yanayoashiria uvunjifu wa amani nchini, Kupitia maneno yake Rais Samia alijikita kulitaka jeshi la polisi kuboresha utendaji wa jeshi hilo na kudhibiti ukiukwaji wa sheria na haki.

Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kulinda maadili na kusimamia sheria kwa uadilifu, akitoa maagizo mahsusi kwa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Matukio ya Utekaji na Mauaji Yanayohusiana na Imani za Kishirikina.

Katika hotuba yake, Rais Samia aligusia kwa kina masuala yanayohusiana na utekaji na mauaji ambayo yamekuwa yakihusishwa na imani za kishirikina. Alieleza kuwa serikali imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu visa vya mauaji na utekaji wa kikatili, ikiwemo mauaji ya watoto albino kwa kukatwa viungo, wazazi kuuawa na watoto, na watoto kuua wazazi wao. Rais Samia amekemea vikali ukimya wa jamii na vyombo vya dola kuhusu matukio haya na kusisitiza kwamba hatua kali lazima zichukuliwe dhidi ya wahusika ili kukomesha vitendo hivi vya kikatili.

Maagizo kwa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Rais Samia aliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha halihusiki na ukiukwaji wa sheria na haki, akisisitiza umuhimu wa maadili katika utekelezaji wa majukumu yao. Alieleza kwamba serikali itatekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwa ukamilifu. Aidha, alihimiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuimarisha utendaji wa polisi na kudhibiti uhalifu kwa ufanisi zaidi.

Usalama Barabarani na Miradi ya Maendeleo

Katika jitihada za kuboresha usalama barabarani, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa ukaguzi wa magari haraka ili kupunguza ajali za barabarani. Aliagiza kuhakikisha miradi kama vile mradi wa miji salama na doria barabarani inatekelezwa kikamilifu. Hii ni sehemu ya jitihada za serikali za kuboresha usalama wa wananchi na kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikisababisha madhara makubwa.

Kukabiliana na Taarifa za Uongo Mtandaoni.

Rais Samia alisisitiza pia umuhimu wa kukabiliana na tatizo la watu wanaozusha habari za uongo mtandaoni. Ameeleza kuwa taarifa za uongo zinaweza kuchochea uvunjifu wa amani, kupotosha umma, na kuzorotesha hali ya usalama. Ameitaka jamii na vyombo vya dola kuwa makini na taarifa hizi na kuchukua hatua za haraka.

Rais Samia amegiza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuanzisha mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti wa habari za uongo, huku akisisitiza kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika wa kueneza taarifa zisizo za kweli.

Heshima kwa Askari Polisi Wastaafu.

Katika hatua ya kuheshimu mchango wa askari polisi, Rais Samia alitunuku vyeti vya pongezi kwa askari polisi wastaafu kumi waliotumikia jeshi hilo kwa uaminifu na uzalendo tangu kabla ya uhuru. Hii ni hatua ya kuonyesha shukrani kwa huduma zao na kuhamasisha vijana kuiga mfano wao.

Hitimisho.

Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan inadhihirisha dhamira yake ya dhati ya kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi, kulinda haki na usalama wa wananchi, na kuhakikisha matumizi ya teknolojia yanachangia katika kuimarisha utendaji wa kisheria. Rais Samia ameonyesha njia wazi ya hatua zitakazochukuliwa ili kukabiliana na changamoto zinazokabili nchi, huku akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na maadili katika utendaji wa majukumu ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *