Rais-wa-Jamhuri-ya-Muungano-wa-Tanzania-Mhe.-Samia-Suluhu-Hassan-akizungumza-na-wanahabari-juu Rais-wa-Jamhuri-ya-Muungano-wa-Tanzania-Mhe.-Samia-Suluhu-Hassan-akizungumza-na-wanahabari-juu

ZIARA YA DKT. SAMIA KATIKA MKUTANO WA AU, KUIMARISHA UCHUMI, UWEKEZAJI NA HUDUMA KWA WANANCHI

Na Mwandishi wetu,

Ripoti ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia tarehe 14–15 Februari 2026, imeonesha wazi maendeleo makubwa ya Tanzania katika sekta muhimu za maji, afya na biashara, sambamba na nafasi ya kipekee ya nchi yetu katika diplomasia ya kiuchumi barani Afrika.

Tuanze na Ajenda ya Maji Afrika 2026 yenye kuelezea Dhamira ya Upatikanaji Endelevu wa Maji Safi Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Kundo Andrea Mathew, ameeleza wazi nia na makusudio ya Rais Dkt. Samia kuongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo, uliotangaza rasmi mwaka 2026 kuwa Mwaka wa Maji Afrika.

Kauli mbiu ya mwaka huu inahimiza upatikanaji endelevu wa maji safi na mifumo salama ya usafi wa mazingira, hatua inayounganisha malengo ya ajenda ya Afrika 2063 “Afrika Tuitakayo” na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Wakati tunapeleka ajenda zetu kimataifa Ripoti inaendelea kuonesha kwamba Tanzania imefikia mafanikio makubwa katika sekta ya maji, ambapo upatikanaji wa maji safi na salama umefikia asilimia 85.2 vijijini na asilimia 95 mijini.

Utekelezaji wa kauli mbiu ya mwaka unalenga kuimarisha rasilimali za maji kupitia maboresho ya bodi za maji za mabonde 9, mamlaka 85 ya maji, RUWASA, maabara 17 za ubora wa maji na Mfuko wa Taifa wa Maji. Zaidi ya hayo, tutakukumbuka kuwa Rais Dkt. Samia alitunukiwa Tuzo ya Rais wa Kimataifa wa Ubunifu wa Mabadiliko katika Sekta ya Maji 2025 na Tuzo ya Kinara wa Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi kutoka WaterAid, tuzo hizi zinaaashiria heshima juu ya mchango wake wa dhati katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na mifumo bora ya usafi wa mazingira.

Katika TEHAMA kwenye Sekta ya Afya: Ripoti pia inaonesha kuwepo kwa jitihada za dhati kupitia serikali ya awamu ya sita kuimarisha sekta ya afya kwa kutumia teknolojia na TEHAMA, hatua inayoongeza ufanisi, kupunguza makosa ya kibinadamu na kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi za huduma za afya.

Kwa sasa Hospitali za wilaya na mikoa tayari zimeboreshwa na vifaa vya kidijitali ikiwemo Digital X-Ray, Ultrasound, CT-Scan na MRI, hatua inayowawezesha wagonjwa kupata huduma bora na haraka.

Huduma za Dawa na uwekezaji wa vifaa tiba: Katika uwasilishaji wa ripoti, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, pia ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia kwa upendo aliidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 126 kwa ajili ya upatikanaji endelevu wa dawa muhimu, ikiwemo ARVs baada ya baadhi ya washirika kutishia kujitoa katika utoaji misaada.

Hatua hii inadhihirisha dhamira ya Mhe Rais ya kulinda afya za wananchi na kujitegemea katika sekta nyeti ya afya, huku pia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya AfCFTA na maono ya Ilani ya CCM 2025–2030.

Zaidi ya hayo, jambo zuri ni kwamba mkutano wa AU umehimiza nchi zote kuongeza bajeti ya afya hadi asilimia 15 ya bajeti ya taifa, hatua itakayosaidia kupunguza utegemezi wa misaada ya nje na kuhakikisha huduma bora na endelevu zinapatikana kwa wananchi.

Uanzishaji na Uimarishaji wa Viwanda vya Dawa: Katika mambo mengine ambayo yametiliwa mkazo na mkutano wa AU ni suala la umuhimu wa kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba barani Afrika.

Hii ni hatua muhimu ya usalama wa taifa, kwani inapunguza utegemezi wa nje na kuhakikishia upatikanaji wa dawa kwa wakati unaohitajika. Wakati mawazo hayo yanatolewa Rais wetu alikwisha ona mbali na Tanzania tayari imeanza kupiga hatua mapema katika eneo hili, ikiwa ni pamoja na uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu mahsusi kusimamia mradi wa viwanda vya dawa, huku ikilenga kufikia asilimia 70 ya uzalishaji wa ndani ifikapo 2030.

Biashara ya Kimataifa na Fursa za AfCFTA: Tanzania pia imejipanga kunufaika kikamilifu na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), ambalo linatoa fursa kubwa ya kukuza uzalishaji, kupanua masoko ya bidhaa za ndani na kuimarisha uchumi wa Taifa.

Ripoti imeonesha kwamba Tanzania tayari imeshafikia maandalizi mazuri katika maeneo manne ya kipaumbele: kilimo-biashara, dawa na vifaa tiba, usafirishaji na biashara ya kidigitali.

Zaidi ya hayo, mauzo ya nje ya Tanzania yameongezeka kwa mara mbili katika miaka mitano iliyopita, hasa kutokana na sekta ya utalii na usafirishaji. Hatua hizi zinaonesha ushawishi wa moja kwa moja wa Rais Dkt. Samia katika kukuza soko la kimataifa na kuvutia uwekezaji.

Nafasi ya Kipekee ya Tanzania Kijiografia na Kiuchumi Kama tunavyojua kuwa Tanzania ipo katika nafasi ya kipekee barani Afrika, ikiwa sehemu ya mnyororo wa kibiashara wa EAC na SADC, ikichangia kuunganisha biashara na usafirishaji wa mizigo barani. Bandari za Tanga na pipeline ya mafuta zinaimarishwa na kupanuliwa, hatua inayosaidia kusafirisha bidhaa nje kwa urahisi na usalama, huku ikihakikisha miundombinu muhimu ya uchumi inalindwa.

Hitimisho

Ripoti hii ya ziara ya Rais Dkt. Samia katika AU inaonesha wazi mafanikio makubwa ya Tanzania katika sekta za maji, afya, dawa na biashara, sambamba na nafasi ya kimkakati ya nchi katika diplomasia ya kiuchumi barani Afrika. Hatua hizi zinathibitisha dhamira ya Serikali ya kuimarisha ustawi wa wananchi, kupanua fursa za kiuchumi, na kuendesha sekta muhimu kwa uwajibikaji na ufanisi, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya 2050 na ajenda ya Afrika 2063.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *