RAIS SAMIA ZIARANI KATAVI. RAIS SAMIA ZIARANI KATAVI.

ZIARA YA RAIS SAMIA KATAVI, KUFUNGUA FURSA HIZI ZA KIUCHUMI NA MAENDELEO.

Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Leo, tarehe 12 Julai 2024 anatarajia kuanza ziara ziara muhimu katika Mkoa wa Katavi, mojawapo ya mikoa mikubwa na yenye rasilimali adimu magharibi mwa nchi.

Mkoa huu, ilianzishwa rasmi mwaka 2012 kama sehemu ya juhudi za serikali kusogeza huduma za kiutawala na kiuchumi karibu na wananchi, unajivunia ardhi yenye udongo wenye rutuba, inayowezesha kilimo cha mazao mbalimbali kama mahindi, mihogo, na matunda.

Historia ya mkoa inaonyesha mchango wake muhimu katika uchumi wa Tanzania kupitia sekta za kilimo, ufugaji, na uvuvi. Wananchi wa Katavi, wanaojishughulisha na shughuli hizi za msingi za kiuchumi, wanatarajia ziara hii ya Mheshimiwa Rais kuleta maendeleo endelevu na fursa za kiuchumi zaidi.

Kwenye ziara hii ambayo inatarajiwa kwenda hadi tarehe 15 Julai Mheshimiwa Rais atapata fursa ya kukagua miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Usafiri, ambayo ni sehemu muhimu katika kuimarisha mawasiliano na kukuza biashara.

Pia, atazindua miradi ya kuhifadhi mazao na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa. Hatua hii ni muhimu katika kuboresha usalama wa chakula na kustawisha kilimo cha mkoa wa Katavi.

Miongoni mwa miradi muhimu ambayo Mheshimiwa Rais anatarajia kuikagua ni pamoja na ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Mpanda na ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa, hatua zinazolenga kuimarisha huduma za afya na usafiri.

Zaidi ya hayo, Rais atazindua bandari mpya ya Karema, ikionyesha dhamira ya serikali katika kuendeleza miundombinu ya usafirishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi katika eneo hilo.

Pamoja na juhudi zake za kuimarisha miundombinu, Mheshimiwa Rais amejitolea katika kufanya mabadiliko makubwa katika miundombinu ya umeme, ambapo pia atafanya ukaguzi kwenye kituo cha kupoozea umeme cha Mlelele. Hatua hii ni sehemu ya mipango ya serikali ya kuongeza upatikanaji wa nishati safi na kuunga mkono maendeleo ya viwanda na biashara katika mkoa.

Kuthibitisha hilo hivi karibuni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko aliagiza Mkoa wa Katavi kuingizwa katika matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa ifikapo Septemba mwaka huu.

Kwa wananchi wa Katavi, ziara hii ni zaidi ya ziara kiserikali tu bali ni ishara ya dhamira thabiti ya serikali ya kuleta maendeleo endelevu na usawa wa kijamii. Matarajio ya wananchi wa Katavi ni kwamba ziara hii itawaletea maisha bora kupitia fursa za ajira, huduma bora za afya na elimu, na miundombinu imara ya usafirishaji na nishati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *