RAIS SAMIA ATAMBUULIWA KWENYE ORODHA YA WANAWAKE WENYE USHAWISHI MKUBWA 2025 RAIS SAMIA ATAMBUULIWA KWENYE ORODHA YA WANAWAKE WENYE USHAWISHI MKUBWA 2025

RAIS SAMIA ATAMBULIWA KWENYE ORODHA YA WANAWAKE WENYE USHAWISHI MKUBWA 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ametajwa katika orodha ya Wanawake 100 Wenye Ushawishi Mkubwa Afrika kwa mwaka 2025 (100 Most Influential African Women) iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya Avance Media.

Tuzo hiyo inatambua wanawake waliotoa mchango mkubwa katika uongozi, maendeleo ya kijamii, ubunifu na mageuzi barani Afrika pamoja na diaspora.

Kwa mujibu wa Avance Media, orodha ya mwaka huu imejumuisha viongozi wanawake wa ngazi za juu wakiwemo marais wawili wa kike, makamu wa marais sita, Waziri Mkuu mmoja, Naibu Katibu Mkuu mmoja wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Naibu Mwenyekiti mmoja wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Hii inaonesha hatua kubwa ya kihistoria katika kuimarika kwa nafasi ya wanawake katika uongozi wa Afrika na majukwaa ya kimataifa, ikiashiria mchango mkubwa wa bara hili katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Miongoni mwa waliotajwa katika orodha hiyo ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Ngozi Okonjo-Iweala; Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan; msanii na mwanaharakati aliyeshinda tuzo ya Grammy, Angélique Kidjo; mwanaharakati wa Togo na mtetezi wa teknolojia ya fedha Fariba Nabourema; pamoja na Dkt. Rasha Kelej, Mkurugenzi Mtendaji wa Merck Foundation.

Mwanzilishi wa Avance Media, Prince Akpah, ameeleza kuwa lengo la uchapishaji wa orodha hiyo ni kuhamasisha usawa wa kijinsia na kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya Afrika.

Ameongeza kuwa kwa kuangazia simulizi za wanawake hawa wenye ushawishi, jamii na taasisi zinahamasishwa kufanya mageuzi ya sera, kuboresha mifumo ya kiutawala na kuanzisha juhudi za msingi zitakazowezesha wanawake na wasichana kote barani Afrika.

Vigezo vya uteuzi kwa orodha hiyo vilijumuisha ubora wa uongozi na utendaji kazi, mafanikio binafsi, mchango katika kusambaza maarifa, uwezo wa kuvunja mifumo iliyopo (status quo), pamoja na kuonesha sifa za mwanamke wa Kiafrika aliyefanikiwa na mwenye athari chanya kwa jamii.

Avance Media imeeleza kuwa kutambuliwa kwa Rais Samia ni ishara ya mchango wake mkubwa katika kuimarisha uongozi wa wanawake barani Afrika na kuendelea kufungua fursa mpya kwa wanawake wa Kiafrika na diaspora kupitia sera, diplomasia na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Orodha kamili na wasifu wa wanawake 100 wenye ushawishi mkubwa Afrika inapatikana kupitia tovuti rasmi ya Avance Media: http://100women.avancemedia.org

#AvanceMedia#100MIAW#100MostInfluentialAfricanWomen

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *