MIAKA 60 YA MUUNGANO: MVUTANO NA JITIHADA ZA KUDUMISHA UMOJA.

Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, tarehe 26/4/2024 kumekuwa na mjadala mkali unaondelea katika mitandao ya kijamii kuhusu usalama wa Muungano huo. Hoja zinazojitokeza zimegawanya maoni ya wananchi na viongozi wa kisiasa, huku kila upande ukitetea msimamo wake.

Nakurudisha nyuma kidogo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa Aprili 26, 1964 ikiwa ni Muungano wa Mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964 huko Zanzibar.

Muundo wa Muungano wa Tanzania kama ulivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, una vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji ambavyo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ambavyo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Zanzibar; na vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ambavyo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Muungano huu ulioasisiwa 1964 kati ya Tanganyika na Zanzibar ulikusudiwa kuwa nguzo ya umoja na mshikamano katika kuleta maendeleo ya pamoja kwa pande zote mbili. Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na wasiwasi kuhusu uthabiti wa Muungano huo, hasa kutokana na hoja zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na wananchi kwa ujumla.

Mzozo uliopamba moto hivi karibuni ulianzishwa na Mbunge wa Jimbo la Konde Visiwani Zanzibar, Mhe. Mohammed Said, alipotoa wito kwa serikali kurejesha utaratibu wa kutumia hati za kusafiria kuingia Zanzibar, hata kwa wananchi wa Tanzania Bara. Hoja yake ililenga kuwalinda Wazanzibari kwa kuzuia msongamano wa watu ambao unaweza kuhatarisha rasilimali na mazingira ya visiwa hivyo.

Mbunge Mohammed alitoa kauli hiyo Bungeni akichangia hoja katika Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira

Hoja hii imepokelewa kwa namna tofauti na jamii. Wapo wanaoiona kama hatua muhimu ya kulinda usalama na ustawi wa kiuchumi kwa Wazanzibari pamoja na hifadhi ya mazingira ya Zanzibar, huku wengine wakiona ni njia ya kuigawa nchi na kuleta utengano.

Hata hivyo, tukumbuke kuwa, kati ya Sababu za kuwepo kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kutokana na mahusiano ya karibu na yakihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika Nyanja mbali mbali kama vile udugu wadamu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu ya kisiasa hususani baina ya vyama vya TANU na ASP.

Kwa kuzingatia mambo ya msingi ya muungano, ni ukweli kwamba Tanzania bara na Zanzibar inaunganishwa na mambo 22 ya muungano yaliyoorodheshwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Moja ya mambo hayo ni suala la Uraia, Sheria inayotumika ambayo ni sheria namba 6 ya mwaka 1995 ilitungwa ili kufuta sheria mbali mbali zilizohusu uraia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuleta mkanganyiko kwenye suala la Uraia.

Kwani, Kwa kipindi kirefu tangu kuasisiwa kwa Muungano, utambulisho wa raia wa Tanzania na wasio raia ulikuwa unafanyika kwa kutumia Hati za Kusafiria, Hati za Vizazi na Vifo na Serikali za Mitaa (nyumba kumi-kumi).

Mpaka Tarehe 30 Julai, 2008, Serikali ilipounda Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (National Identification Authority – NIDA) kwa Hati Maalum ya Rais, Tangazo la Serikali Na.122.

Majukumu ya Mamlaka hii ni kuhakiki uraia wa watu waishio nchini na kusajili taarifa zao, kuwapatia vitambulisho na kutengeneza Daftari la Kudumu lenye taarifa za utambuzi wa watu ambazo pia zitatumiwa na wadau wengine pamoja na kujenga mfumo wa utambuzi na usajili wa watu kitaifa.

Ukiachana na suala la uraia, jambo jingine lililoainishwa ni suala la Uhamiaji. Mnamo Mwaka 1995, Sheria zilizokuwa zinasimamia majukumu ya uhamiaji, Tanzania Bara na Zanzibar zilifutwa na kutungwa Sheria ya Uhamiaji Na.7 ya mwaka 1995 na Kanuni zake za mwaka 1997. Aidha, Sheria zilizokuwa zinasimamia masuala ya uraia ziliunganishwa na kuwa Sheria ya Uraia Namba 6 ya mwaka 1995 na Kanuni zake za mwaka 1997.

Ili kuboresha huduma za pasipoti, Serikali ilitunga Sheria ya Kusimamia Utoaji wa Pasipoti na Hati za Kusafiria (Tanzania Passport and Travel Document Act) Sura Namba 42 na Kanuni zake za mwaka 2004.

Ni muhimu kutambua kuwa serikali, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imejitahidi kudumisha umoja kupitia vipaumbele vyake vinne: Upatanisho, Uthabiti, Mageuzi, na Kujenga Upya. Ambavyo vinagusa moja kwa moja suala zima la muungano. Vipaumbele hivi vimekuwa dira katika kushughulikia changamoto za ndani na nje, kama vile janga la COVID-19 na migogoro ya kisiasa.

Kupitia vipaumbele hivi, serikali inawapa nafasi wananchi na wana siasa kushiriki katika kuleta suluhisho kwa changamoto zinazowakabili.

Ni muhimu kuelewa kuwa mjadala kuhusu Muungano haupaswi kuleta mgawanyiko, bali unapaswa kutumika kama fursa ya kujenga uelewa na suluhisho la pamoja. Kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano, ni wakati wa kutafakari jitihada zilizofanywa na kuendeleza pasipo kuathiri umoja na mshikamano kupitia rasilimali zetu tulizobarikiwa kwa manufaa ya pande zote mbili.

Hivyo basi, ni wakati wa kufanya mjadala wa kina na wa kujenga ili kuhakikisha kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaendelea kuwa imara na wenye manufaa kwa wananchi wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *