Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa matanki ya mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam tarehe 3 Machi 2026, hatua inayokuja wakati wa mzozo mkali wa kijeshi kati ya Marekani, Israel na Iran ambao umezua hofu kubwa ya usalama wa nishati duniani.

Mradi huu wa Shilingi bilioni 701.8 (kulingana na ripoti), unaotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) chini ya Wizara ya Uchukuzi, unalenga kujenga matanki 15 yenye uwezo wa jumla wa mita za ujazo 378,000 ikiwa ni pamoja na dizeli (162,000 m³), petroli (135,000 m³) na Jet A1 (81,000 m³). Hadi sasa, utekelezaji umefikia asilimia 41, na unatarajiwa kukamilika Februari 2027.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa mradi huu ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya kuimarisha miundombinu ya bandari na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kati.

Vilevile Mhe Rais ameagiza kuongezwa kwa uwezo wa Akiba ya Kimkakati ya Hifadhi ya Mafuta (National Strategic Petroleum Reserves) ili kukabiliana na misukosuko ya soko la kimataifa, pamoja na matumizi ya mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji wa shehena za mafuta ili kuongeza uwazi na kulinda mapato ya Taifa.
Wote wakati tunaendelea kushuhudia mzozo kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran uliozuka na unaendelea kufikia Mwezi huu wa Machi 2026, ukiachana na mashambulizi mbali mbali katika sehemu tofauti, inajumuisha pia mashambulizi ya meli na miundombinu ya nishati katika Ghuba la Uajemi.

Hali ambayo imesababisha kufungwa kwa muda kwa (Strait of Hormuz), mfereji muhimu unaopitisha karibu asilimia 20 ya mafuta na gesi ya dunia.
Matokeo ya vita hii ni kuongezeka kwa bei za mafuta duniani, ambapo Bei ya Brent crude imepanda kutoka karibu $73 hadi zaidi ya $80-83 kwa pipa katika siku chache, na hofu kuwa ikiendelea kufungwa kwa Hormuz inaweza kufikia $100 au zaidi, na hivyo kusababisha mfumuko wa bei na uchumi mdogo kimataifa.

Kwa nchi kama Tanzania, ambayo inategemea kuagiza mafuta mengi kutoka Mashariki ya Kati (kupitia bandari ya Dar es Salaam), hali hii pia inatuathiri kutokana na kupanda kwa bei za mafuta kupanda ndani ya nchi, kuathiri gharama za usafiri, uzalishaji na maisha ya kila siku.
Ucheleweshaji wa shehena, gharama za juu za bima ya meli, na upungufu wa usambazaji.
Na Hapa ndipo serikali inakusudia kupunguza changamoto kama hizi huko mbeleni kupitia mradi wa ujenzi wa matanki yaliyozinduliwa na Mhe rais Samia ili kuongeza akiba ya kimkakati.

Baada ya uzinduzi huo, tunatajia kuwa na Ongezeko la uwezo wa kuhifadhi mafuta kutoka mita za ujazo milioni 1.05 hadi 1.43 ( sawa na ongezeko la asilimia 35.9) ambalo litatoa “buffer” ya miezi kadhaa ya matumizi, hivyo kupunguza hatari ya upungufu wa mafuta wakati wa migogoro ya kimataifa kama tunavyoshuhudia kufungwa kwa njia muhimu za usafirishaji kama Hormuz.
Mradi huu pia, utapunguza muda wa kushusha shehena za mafuta kutoka siku 22 hadi siku 7 kwa meli moja, na hivyo kuokoa takriban $25,000 kwa siku kwa tozo za ucheleweshaji
Kwa kuwa tutakuwa na hifadhi kubwa ya mafuta na ya kisasa, Tanzania itaweza kudumisha utulivu wa bei za mafuta hata wakati bei duniani zinapopanda ama pale usambazaji unaposuasua. Hii itasaidia katika sekta za uzalishaji, kilimo, na usafiri, na hivyo kuzuia mfumuko wa bei na kudumisha ukuaji wa uchumi.

Kupitia mradi huu pia Tanzania itakuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi na kusambaza mafuta kwa nchi jirani (kama Zambia, Malawi, DRC), na hivyo kuimarisha nafasi yake kama lango la nishati katika ukanda.
Katika nyakati kama hizi ambazo nchi mbali mbali zinaingia kwenye mizozo ya mara kwa mara na kutikisa soko la mafuta duniani, uamuzi wa Rais Samia wa kuwekeza katika miundombinu hii unaonyesha maono ya muda mrefu ya kulinda uchumi wa Tanzania dhidi ya misukosuko ya kimataifa, na kuifanya nchi iwe na uhakika mkubwa wa nishati na ushindani wa kikanda.

Hii ni hatua muhimu na ya kimkakati katika kujiandaa na changamoto za usalama wa nishati kwa siku zijazo.