Kwa kawaida, bubu huwa hasemi, haongei wala hasikiki. Na ni ukweli kwamba si jambo la kawaida kufikiria kuwa bubu anaweza kusimama na kusema maneno ambayo yatakuwa na uzito. Hii ni kwa sababu bubu hasikii, hasemi, wala hawezi kusikika anapozungumza.
Lakini, niamini iko siku moja ambayo, kwa sababu ya yote yanayosemwa, Bubu hulazimika huamka na kujibu kwa nguvu, baada ya kuvumilia madhila, kuvunjwa heshima, kupoteza utu na kupuuzwa.
Hali hii hujitokeza pale anapovunjiwa heshima, kukandamizwa, au kupuuzwa mara kwa mara, huku akiwa hajawahi kuvunja staha kwa wengine. Lakini inapofika hatua hiyo, lazima sauti yake isikike, kwani ni sauti yenye uchungu wa mwana aliyekandamizwa, kufinywa na kubanwa pumzi. Ni sauti ya mtu aliyevunjwa utu wake.
Tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipochukua madaraka baada ya kifo cha Dk. John Magufuli, amekuwa kiongozi mwenye haiba ya upole, utulivu, na uvumilivu, sifa hizi amekuwa nazo tangu hajawa Rais. Hivyo, hawezi kubadilika ghafla na kuiga ukorofi wa wengine. Tabia, mwenendo na maumbile ya mtu hayana dawa. Ukiwa mbaya, ni mbaya. Na ikitokea umejaliwa tabia njema, huwezi kubadilika kuwa katili au jeuri. Kila mtu ameumbwa kwa tabia na mwenendo wake.
Hata hivyo, baadhi ya watu wamechukulia upole wake kama udhaifu. Wanasiasa na wapinzani wake, kwa nyakati mbalimbali, wamejaribu kumdharau, wakiamini kuwa yeye ni dhaifu kwa sababu tu ya haiba yake ya upole na staha.
Lakini ukweli ni kwamba Rais Samia si mgeni katika siasa wala uongozi. Amejenga uzoefu wa miaka mingi na amepitia changamoto mbalimbali, akifika hatua ya kuwa Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa Nchi. Aliwahi kusema mwenyewe katika moja ya hotuba zake kwamba upole wake haimaanishi kushindwa kutekeleza majukumu yake kikatiba.
Wale wanaomdharau na kumchukulia kwa kebehi wanakosea, kwani ni sawa na mtu anayejaribu kumchezea simba sharubu au anayemchokoza nyoka wa kijani, mpole lakini mwenye sumu kali. Ikifika wakati bubu anapoamua kusema, usifikiri amesema kwa hiari. Amesema kwa sababu amelazimishwa na mazingira. Hii ni falsafa ya aina ya uongozi anayowakilisha — uongozi wa ustaarabu na maelewano.
Baadhi ya wanasiasa walidhani kuwa kuonyesha ustaarabu na kuwashirikisha wapinzani ni ishara ya udhaifu. Lakini hilo ni kosa kubwa. Rais Samia hakuwaelewa wapinzani kama maadui, badala yake ameona ni muhimu kuleta umoja na mshikamano wa kitaifa. Wapo wanasiasa waliowahi kukutana na changamoto kubwa, hadi kufikia kukimbia nchi yao, wakikumbwa na kesi za kutisha, lakini leo wamepoteza kumbukumbu ya hayo yote. Wanajaribu kumjaribu Rais Samia na kupima uvumilivu wake.
Hata hivyo, wale wanaodhani kuwa Rais Samia ni kiongozi asiye na meno wanajidanganya. Siku akiamua kuchukua hatua, wale waliokuwa wakimdharau wataona nguvu yake. Sheria zinazowalinda zinaweza kutumika tena wakati wowote, na hakuna anayepaswa kuzidharau.
Nihitimishe kwa kusema kuwa upole si udhaifu, na Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi anayejua kupima mambo. Wanaomdharau wajiandae kwa maamuzi yenye nguvu, kwani bubu, akiamua kusema, husema kwa uchungu wa mwanae.
Credit>Jamhuri.