Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kimekuwa na sera ya mageuzi, kikijinasibu kuwa mwokozi wa watanzania, katika nyanja mbali mbali na kuwa na shauku ya kupata madaraka kwa muda mrefu kimeanza kutuonesha makucha yake, huku kikitushangaza kutokana na kuzigeuka zilizokuwa agenda zake za muda mrefu, kupitia kwa viongozi wakubwa kabisa na vigogo kutoka chama hicho.
Wale Waliokuwa wakitetea uwazi katika matumizi ya fedha za umma, sasa wanakataa kuulizwa maswali kuhusu fedha za kampeni kama vile Join The Chain.
Wale waliokuwa wakihubiri umuhimu wa mabadiliko, uwajibikaji wa viongozi, na kupinga kukaa madarakani kwa muda mrefu, sasa wanaunga mkono mwenyekiti aliyekalia kiti kwa zaidi ya miongo miwili huku wakipinga kila anayependekeza mabadiliko.
Waliokuwa wakisema hakuna uchaguzi mkuu bila mabadiliko, sasa wanampinga mgombea anayetaka mwelekeo mpya wa chama, na kumtusi kwa mambo mbali mbali.
Waliokuwa wakipinga uongozi wa mabavu, sasa wanampigia debe kiongozi wa chama aliyeshindwa kukabidhi kijiti.
Wakati wa kampeni za mwaka 2020 CHADEMA ilituaminisha katika mbio za urais kuwa wameweka mgombea shupavu, kiongozi mwenye kuhamasisha mabadiliko, na kiongozi mwenye imani kubwa na watanzania. Leo tunashangazwa wakituambia kuwa, mgombea huyo alikuwa tu wa kujaza nafasi, wala sio kwa sababu ya ushindi, wala ki uhalisia hakuwa hata na chembe ya sifa za kuwa rais.
Waliokemea vikali propaganda za serikali na vyombo vya habari vya umma, na vingine, leo hii wanatumia vyombo hivyo hivyo kupiga kampeni na kujinadi kwa wananchi na wanachama.
Waliopinga mawazo ya kudharau wananchi kama alivyofanya waziri wa serikali aliyesema wananchi wahamie nchi jirani kama hawakubaliani na sera za kodi, sasa wanawaambia wanachama waondoke chama kama hawakubaliani na mwenyekiti.
Sio hayo tu, tunashuhudia pia Waliokemea “maigizo” kusifia na kuonesha mema kwa watawala, sasa wanaratibu maandamano ya pikipiki na makundi mengine kwa ajili ya kufanikisha ajenda zao na tena wengine wakidiriki kufika mbali na kumuita kiongozi wao ALFA na OMEGA.
Wanachama waliozunguka nchi nzima kwa wananchi maskini na bakuli la michango mikononi ili kuendesha chama, sasa wanajitapa kwamba chama chao kimejaa utajiri.
Wale waliokuwa wakikemea juhudi za kulazimisha viongozi wa serikali kubaki madarakani, wao kwa wao leo hii wanaandaa maandamano feki “kushinikiza” mwenyekiti wao agombee tena na tena.
CHADEMA, kilichoonekana kama chombo cha mabadiliko kwa muda mrefu, sasa kimefika mahali pa kutathmini upya misingi yake. Ni ukweli usiojificha kuwa hapa hakuonekani uwepo wa mabadiliko wala viapo walivyokuwa wakituaminisha, siyo tu nje ya chama, bali pia ndani ya chama inaonekana hakuna demokrasia wanayoizungumzia.
Kwa pamoja, Watanzania wanapaswa kuhoji: Je, chama hiki kimebaki kuwa taa ya mabadiliko au kivuli cha yale waliokuwa wakiyapinga?
Credit> Mwana Halisi.