ELIMU YACHOCHEA UHAMAJI WA HIARI KWA WANANCHI WA NGORONGORO

Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro

Elimu juu ya kuhama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro imeendelea kuleta mafanikio makubwa, huku wananchi wakielewa na kuchukua hatua za kuhama kwa ridhaa ili kuimarisha uhifadhi.

Katika hatua ya hivi karibuni, kaya 28 zenye watu 130 na mifugo 346 ziliripotiwa kuhamia katika vijiji vya Msomera, Handeni na Meatu. Taarifa hizi zilitolewa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, Gloria Bideberi, ambaye alifafanua kuwa kati ya kaya hizo, 26 (watu 119 na mifugo 329) zilihamia Msomera, huku kaya mbili (watu 11 na mifugo 17) zikihamia kijiji cha Makan, Meatu mkoani Simiyu.

Gloria alieleza kuwa tangu Juni mwaka 2022 hadi sasa, kaya 1,655 zenye jumla ya watu 9,976 na mifugo 40,397 zimehama kwa hiari kutoka Ngorongoro. Aliongeza kuwa, wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiari huhamishwa ndani ya kipindi cha wiki mbili, na serikali imekuwa ikihakikisha uhamisho unafanyika haraka.

“Serikali imeendelea kutuwezesha. Hata pale tunapopata idadi ndogo ya kaya zinazotaka kuhama, tunazihamisha kwa haraka bila kuchelewa,” amesema Gloria.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dk. Alex Lobora, aliwapongeza wananchi wa Ngorongoro kwa uamuzi wao wa kuhama kwa hiari ili kupisha juhudi za kuimarisha uhifadhi na kuboresha maisha yao nje ya hifadhi. Alisema kuwa hatua hii inaonesha matokeo chanya katika juhudi za kuokoa hifadhi kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Ngorongoro ni eneo la urithi wa dunia, linaloendelea kuvutia watalii na kuingiza mapato kwa serikali. Nawashauri muendelee kuwa mabalozi, mkishawishi ndugu zenu waliobaki kuhama ili kulinda wanyamapori, mazingira, misitu, na urithi wa malikale wa Ngorongoro,” alisisitiza Dk. Lobora.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Lilian Maguma, alieleza kuwa mchakato wa uhamisho umefanyika kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi kupitia elimu juu ya umuhimu wa kuhama kwa hiari ili kusaidia juhudi za uhifadhi. Aliongeza kuwa maeneo ya malisho yaliyotengwa ni ya kutosha, ambapo Msomera kuna hekta 22,000, Saunyi hekta 9,000, na Kitwai hekta 53,000, ambayo yataweza kuhudumia mifugo ya wananchi wanaoendelea kuhamia maeneo hayo.

Uhamisho huu unatoa fursa kwa wananchi kuanza maisha mapya, huku wakichangia katika kuhifadhi rasilimali za kitaifa na kuhakikishia vizazi vijavyo mazingira bora na endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *