FAHAMU VIPAUMBELE KUMI VILIVYO BAINISHWA NA WIZARA YA AFYA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2024/2025.

Akiwa Bungeni jijini Dodoma Mhe Ummy Mwalimu, tarehe 13/5/2024 aliwasilisha Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25, Mhe Waziri alionesha wazi mafaniko ya wizara yake kwa mwaka uliopita, ilo sio jambo ambalo ntakupitisha, bali tuangazie malengo mapya ya Wizara inapokwenda kutekeleza na kuboresha huduma za afya nchini katika mwaka mwaka wa fedha 2024/25 upate kufahamu vema matumizi ya bajeti iliyoidhinishwa katika siku ya jana pale bungeni.

Kwanza kabisa Mhe Waiziri Ummy Mwalimu alibainisha vipaumbele kumi vya msingi vya wizara ambavyo imelenga kuhakikisha  vinafanyika katika mwaka wa fedha 2024/2025 ambavyo vinamgusa kila mtanzania, na vipengele venyewe ni kama vifuatavyo.

Kipengele namba moja 1 kilicho ainishwa na Wizara ya afya, ni kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa na vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Taifa.

Kama tunavyofahamu kuwa bado katika nchi zetu zinazoendelea tuna changamoto kubwa ya huduma za kiafya na hii ni kutokana na umasikini Pamoja na teknolojia duni katika vifaa vya kitabibu, kupitia mikakati ya  wizara tunaona wazi imejiwekea lengo la kuhakikisha wanaongeza ubora zaidi katika huduma za kiafya.

Na katika eneo hili Seikali yaa Awamu ya sita kupitia Wizara ya Afya imebainisha wazi jumla ya Shilingi 219,010,767,716.00 zimetengwa kutekeleza afua zifuatazo:-

  • Kununua, kutunza na kusambaza dawa na bidhaa nyinginezo katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya (Shilingi 200,000,000,000.00);
  • Kuimarisha upatikanaji wa damu salama (Shilingi 3,503,771,816.00);
  • Kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini (Shilingi 8,596,534,400.00);
  • Kuimarisha na kuunganisha mifumo ya TEHAMA katika vituo vya kutolea huduma ili kuboresha ufanisi, kuimarisha udhibiti na kupunguza gharama katika utoaji wa huduma za afya (Shilingi 2,000,000,000.00);
  • Kuimarisha ubora wa huduma za Uuguzi na Ukunga katika ngazi zote za kutolea huduma kwa vituo vya umma na binafsi (Shilingi 4,910,461,500.00)

Kipengele namba Mbili 2 kilichozungumziwa katika mikakati ya wizara ya afya kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ni Kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini.

Hili ni eneo ambalo limekuwa likuzua mtafaruku mitandaoni katika siku za hivi karibuni, hususani kwenye suala la BIMA YA AFYA KWA WATOTO, Sasa basi wizara ya Afya imetenga kiasi cha Shilingi 6,000,000,000.00 kutekeleza afua zifuatazo: –

  • Kufanya mapitio ya mkakati wa upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia huduma za Afya;
  • Kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote nchini ikiwemo mfumo wa utambuzi wa wanufaika pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya;
  • Kuanza mchakato wa kuanzisha Chombo cha Kitaifa cha Udhibiti wa bei za huduma za afya katika ngazi zote;
  • Kuimarisha uhai na ustahimilivu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya;
  • Kuimarisha ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika utoaji wa huduma za afya nchini”

Kipaumbele namba tatu 3 ni Kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga;

Katika suala la afya, bado kama nchi inakubwa na Changamoto ya vifo vya wajawazito lakini pia elimu ndogo ya afya ya uzazi, uchache wa vifaa na wauguzi Pamoja na mazingira duni ambayo mara nyingi vinapelekea watanzania kutokupata taarifa na huduma sahihi kwa wakati sahihi na hivyo kuwasababishia changamoto wakati au baada ya huduma za uzazi.

Kwa kulitambua hili serikali ya awamu ya sita kupitia wizara ya afya imejipanga kutatua ama kupunguza zaidi tatizo hili ambapo kiasi cha Shilingi 17,189,250,000.00 kimetengwa kutekeleza afua zifuatazo:-

  • Wizara imejipanga kuhakikisha inanunua na kusambaza dawa muhimu za uzazi salama kama (Magnesium sulphate, Oxytocin, FeFo na SP) pamoja na dawa za uzazi wa mpango, dawa kinga za minyoo, dawa za kuongeza damu, dawa za Malaria, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi;
  • Kuimarisha upatikanaji wa dawa bila malipo kwa ajili ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano ikiwemo dawa za kutibu nimonia na kuharisha;
  • Kujenga, kukarabati na ununuzi wa vifaa tiba vya wodi 100 maalum za watoto wachanga (Neonatal Care Unit – NCU) wagonjwa na waliozaliwa na uzito pungufu.”

Kipengele namba nne 4 ni Kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi nchini; Katika eneo hili serikali imejipanga kuhakikisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalam katika Sekta ya Afya kwa fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi; Kaama tunavyotambua kuwa tunahitaji zaidi matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu lakini pia wagonjwa mahospitalini,

Wizara ya Afya imeona kadhia hii, na serikali imetenga kiasi cha Billioni 89,858,609,000 kwa ajili ua matibabu ya ubingwa na ubingwa Bobezi, hapa nchini kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Waziri Ummy, amesema Serikali inakusudia kuendelea kutoa huduma za matibabu ya Ubingwa na Ubingwa Bobezi katika Hospitali ya Taifa (Muhimbili), Hospitali Maalum, Kanda na Mikoa pamoja na kuanzisha huduma mpya kulingana na mahitaji yaliyopo.

Ametaja mahitaji hayo kuwa ni pamoja na upandikizaji wa figo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa ya Bungando, upandikizaji wa ujauzito kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma

Ameongeza kuwa Serikali inakusudia kuwekeza kwenye vifaa tiba vitakavyowezesha utoaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi ikiwemo ununuzi wa mtambo wa kupima na kutibu moyo (Cathlab) kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na kuendeleza ujenzi wa miundombinu katika Hospitali sita (6) za Rufaa za Kanda za Chato, Mtwara, Mbeya, KCMC, Bugando, Benjamin Mkapa, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi Kigoma na Hospitali 28 za Rufaa za mikoa.

Lakini pia, Amesema eneo jingine linalotarajiwa kuimarishwa na serikali ni uboreshaji wa utolewaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi na kuendeleza ujenzi wa kituo cha matibabu ya Saratani tawi la Taasisi ya Saratani Ocean Road Mbeya, kuanzisha tawi la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Kanda ya Ziwa (JKCI Chato)

Sambamba na hilo liko suala la kuanza hatua za awali za maandalizi ya Taasisi ya Sayansi ya Tiba ya magonjwa ya Ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ili kuimarisha huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu nchini.

Amesema pia kugharamia huduma za matibabu ya ubingwa bobezi ndani ya nchi hususani kupandikiza figo, kupandikiza uloto, kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto na kufanya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu sambamba na kuwajengea na uwezo wataalam wa ndani kutoa huduma hizo kwa umahiri zaidi

Katika hatua nyingine, kwenye eneo hilo Waziri Ummy amesema serikali inakusudia kuanzisha kituo cha umahiri cha upandikizaji uloto na magonjwa ya Damu cha Afrika Mashariki katika Hospitali ya Benjamin Mkapa

Hiyo ikienda sambamba na kuimarisha mifumo ya kielektroniki katika Hospitali zilizoteuliwa ili ziweze kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kupitia Tiba Mtandao (Telemedicine) ndani na nje ya nchi; na kuendelea kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kwa wagonjwa kutoka nje ya nchi (Tiba Utalii).

Kipengele namba tano 5 ni Kuimarisha upatikanaji wa wataalam katika Sekta ya Afya katika fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi.

Kipengele hiki kinaendana moja kwa moja na kipengele namba nne, lengo la serikali  ni kuhakikisha sio kuwa tu na miundombinu iliyokuwa bora, lakini pia kuwa na wataalamu wanaoendana na mabadiliko ya teknolojia katika masuala mazima ya afya. Na katika eneo hili wizara imetenga kiasi cha Shilingi 74,000,000,000 kuteleza afua zifuatazo:-

  • Kuendelea kutoa ufadhili wa mafunzo ndani na nje ya nchi kwa wataalam wa ngazi ya ubingwa na ubingwa bobezi 1,300 (wataalam wapya 600, wataalam wanaoendelea 700) na kufadhili mafunzo ya kada za kati za kimkakati (Shilingi 9,000,000,000.00);
  • Kutoa mafunzo ya afya ya kada za kati katika vyuo vya afya vya umma (Shilingi 10,000,000,000.00);
  • Kugharamia mafunzo kwa vitendo ya watarajali wa kada mbalimbali za afya (Shilingi 54,000,000,000.00);
  • Kujenga na kukarabati miundombinu ya vyuo vya mafunzo ya Afya vya umma (Shilingi 1,000,000,000.00); na
  • Kuanzisha kozi mpya ili kukidhi mahitaji ya sasa ya Sekta ya Afya.

Kipengele namba sita 6 ni Kuimarisha huduma za Afya ya Akili, huduma za utengamao na Tiba Shufaa hususan kwa Watoto, Wazee na Wenye Ulemavu. Ni kweli kabisa changamoto ya afya ya akili imekuwa kubwa kwa miaka ya hivi karibuni, na bahati mbaya zaidi ni wananchi wachache sana tuna uelewa juu ya magojwa haya lakini pia haikuwa kipaumbele sana kwa wataalaamu wetu.

Wizara kwa mwaka huu wa fedha imetenga kiasi cha Shilingi 9,318,528,988.00 kwa ajili ya kukabiliana na matatizo haya nchini, na zitatumika kutekeleza afua zifuatazo;

  • Kutoa elimu kwa umma kuhusu vihatarishi vya afya ya akili na namna ya kukabiliana navyo;
  • Kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya ya akili katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Halmashauri;
  • Kuimarisha upatikanaji wa dawa za afya ya akili;
  • Kuanzisha huduma za afya ya akili kwa njia ya mtandao; na
  • Kuanzisha huduma tatu za utengamao (Fiziotherapia, Tiba Kazi (occupational therapy), Matamshi na Lugha (Speech and language therapy) katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 10;
  • Kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za utengamao katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na kuendeleza utoaji wa huduma za utengamao kuanzisha kituo cha umahiri cha huduma za utengamao;
  • Ununuzi wa dawa, vifaa na vifaa tiba vya kutolea huduma za utengamao pamoja na vifaa saidizi ikiwemo mikongojo kwa wazee;
  • Kuratibu uanzishwaji wa Klabu za Afya za Wazee katika ngazi ya Halmashauri.”

Kipegele namba saba 7 ni Kusimamia Tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya.

Hili ni jambo la msingi sana katika tifa lolote linalohitaji mageuzi ya sekta mbali mbali kwakuwa tafiti zinakuonesha ukubwa wa tatizo na mapendekezo ya kutatua tatizo lililopo, hivyo basi katika eneo hili wizara imetenga kiasi chaShilingi 3,508,968,000.00 kwa ajili ya kutekeleza afua zifuatazo;

  • Tafiti za magonjwa yasiyoyakuambukiza ikiwemo Saratani,
  • Ufuatiliaji wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa,
  • Utafiti juu ya changamoto ya Afya ya Akili,
  • Utafiti juu ya matumizi ya Energy Drink,
  • Utafiti kuhusu Nguvu za Kiume na
  • Utafiti kuhusu dawa za Tiba Asili.

Kipengele namba nane 8 kilicho ainishwa na wizara ya afya katika bajeti ya mwaka 2024/2025 ni kuhakikisha wanaimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa. Hili ni eneo muhimu sana kwa ustawi wa nchi kwakuwa inalenga  kuhakiksha mpango endelevu wa afya bora kwa kila Mtanzania. Katika eneo hili wizara imetenga kiasi cha Shilingi 117,611,588,304.00 zitakazotekeleza afua zifuatazo:

  • Kuendelea kuimarisha utekelezaji wa afua za chanjo kwa kuwafikia watoto (surviving infants) 3,117,564 wenye umri chini ya miaka miwili (2), wasichana 871,429 wenye umri wa miaka tisa (9) na wajawazito 3,298,437 (Shilingi 115,369,238,904.00);
  • Kutekeleza afua za lishe ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhimiza unyonyeshaji na ulishaji sahihi wa watoto, elimu ya lishe kwa jamii na kuimarisha Mpango wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula ambapo ununuzi na usimikaji wa mashine 300 za kuongeza virutubishi (Dozifiers) utafanyika (Shilingi 1,607,700,000.00);
  • Kuimarisha utekelezaji wa afua za usafi na afya mazingira katika jamii, Mipakani, taasisi za umma na binafsi ikiwemo kutekeleza kampeni ya mtu ni afya awamu ya pili (Shilingi 634,649,400.00); na 
  • Kuendeleza utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (Shilingi 1,000,000,000.00)

Kipengele namba tisa 9 ni Kuendeleza na kusimamia afua za Tiba Asili na Tiba Mbadala; Nakurudisha nyuma kidogo, kipindi cha mripuko wa UVIKO 19 tulishuhudia uhitaji na matumizi makubwa ya tiba asili na tiba mbadala, sio jambo la kushangaza lakini moja ya changamoto ambayo tulikutana nayo ni urasimishaji wa tiba hizi hususani katika matumizi kwa wagonjwa.

Hivyo hatuwezi kupingana na ukweli kwamba tunahitaji zaidi kuwekeza nguvu kubwa kusimamia suala zima la tiba hizi.

Tukumbuke pia wakati akiingia madarakani Mhe Rais Samia alikumbana na changamoto ya UVIKO 19 ambayo sio tu iliathiri afya za watanzania lakini pia ilisababisha athari kubwa katika ukuaji wa kiuchumi nchini. 

Hivyo basi katika Kuendeleza na kusimamia afua za Tiba Asili na Tiba Mbadala serikali imetenga kiasi cha Shilingi 1,500,000,000.00 afua zifuatazo:-

  • Kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Tiba Asili na Tiba Mbadala;
  • Kuendeleza huduma za Tiba Asili ikiwemo mashamba ya miti dawa katika mikoa mbalimbali likiwemo shamba la Mzenga B Kisarawe;
  • Kununua ardhi na kufanya usanifu wa ujenzi wa Hospitali maalum ya kitaifa ya kutoa huduma jumuishi za Tiba Asili na Tiba Mbadala;
  • Kuongeza Hospitali zinazotoa huduma jumuishi za Tiba Asili kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa saba (7) hadi kumi na nne (14)”

Kipengele namba kumi 10 kilicho ainishwa na Wizara ya afya ni Kuimarisha upatikanaji wa huduma za magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya mlipuko;

Katika kuhakikisha serikali inaimarisha udhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza, Magonjwa Yasiyoambukiza, Magonjwa ya Mlipuko na Huduma za Afya za Dharura imetenga kiasi cha Shilingi 84,864,241,569.00 kutekeleza afua zifuatazo:-

  • Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kwa kununua na kusambaza vyandarua vyenye dawa kwa jamii, kununua vitendanishi na dawa ili kuwezesha ugunduzi na matibabu ya ugonjwa wa Malaria;
  • Utekelezaji wa Mpango wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma kwa kununua vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na dawa;
  • Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, Homa ya Ini na magonjwa ya ngono nchini kwa kununua vitendanishi vya kupima magonjwa hayo pamoja na dawa kinga na dawa za kufubaza VVU;
  • Kutoa elimu kwa umma kuhusu vichochezi na visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo tabia bwete, uzito uliokithiri, matumizi ya sukari, chumvi, na mafuta kupita kiasi pamoja na kuelimisha kuhusu athari za matumizi ya tumbaku na unywaji wa pombe kupita kiasi;
  • Kuimarisha upatikanaji wa dawa za kutibu magonjwa yasiyoambukiza;
  • Kutoa mafunzo kwa watoa huduma za magari ya wagonjwa (paramedics) kwa kushirikiana na Vyuo vya kati na Vyuo Vikuu nchini; na
  • Kuimarisha Mfumo wa Kitaifa wa Uratibu na Usimamizi wa Afua za Afya ya Jamii ikiwemo kuanzisha Taasisi ya Taifa ya Afya ya Jamii;”

Kwa kuzingatia vipaumbele vilivyotajwa, inaonesha wazi kuwa serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Afya imejipanga kwa njia nzuri kuboresha huduma za afya nchini Tanzania katika mwaka wa fedha 2024/25.

Mpangilio mzuri wa vipaumbele unadhihirisha nia ya serikali ya kufanya maboresho makubwa katika sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na kuzuia magonjwa, kuboresha huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi kitaifa, kuimarisha miundombinu ya ugharamiaji, na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto.

Pia, kipaumbele kimeelekezwa katika kuendeleza wataalamu wa afya, kusimamia tiba asili na mbadala, na kuimarisha huduma za afya ya akili. Kama utekelezaji utafanyika kwa kadri ya malengo ya wizara yalivyo ainishwa, ni ukweli kwamba Hatua hizi zinaashiria jitihada zinakwenda kuboresha afya na ustawi wa wananchi.

Top of Form

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *