HATARI YA MATUMIZI YA NISHATI ISIYO SAFI BARANI AFRIKA; JITIHADA ZA SERIKALI KATIKA KUKABILIANA NA ATHARI HIZO NCHINI.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameshiriki kikao muhimu cha kimataifa kilichojadili suala la Nishati Safi ya Kupikia kwa Afrika. Mkutano huu umefanyika katika Makao Makuu ya UNESCO Jijini Paris, nchini Ufaransa, tarehe 14 Mei 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, katika ushiriki wake ametoa taarifa muhimu kuhusiana na Nishati Safi ya Kupikia kwamba,  licha ya Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu na rasilimali muhimu, bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.

Zaidi ya Waafrika milioni 900 wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia, hali inayochangia uharibifu wa mazingira, upotevu wa bioanuai, na athari za kiafya.

Rais Samia ameelezea kwamba changamoto za upatikanaji wa nishati safi ya kupikia zinahusisha mambo matatu muhimu. Kwanza, katika maeneo ya vijijini, upatikanaji wa nishati safi unakumbwa na changamoto kubwa kutokana na gharama na ugumu wa upatikanaji.

Pili, kwa ujumla, jamii ya kimataifa haijatoa kipaumbele cha kutosha kuhusu suala hili, na hivyo kusababisha upatikanaji mdogo wa ufadhili na uelewa duni wa fursa za kiuchumi zilizopo katika nishati safi ya kupikia. Tatu, kuna uhaba wa ushirikiano wa kimataifa katika kuhakikisha kuwa nishati safi ya kupikia inapatikana kwa kila mtu.

Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kupatikana kwa suluhisho linaloweza kutekelezeka, lenye gharama nafuu, na linaloleta mabadiliko chanya. Ameongeza kwamba kuongezeka kwa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kutaimarisha uwezo wa wanawake kushiriki katika shughuli za kiuchumi zaidi, kupunguza umaskini, na kukuza usawa wa kijinsia.

Kauli yake hii inaashiria dhamira ya serikali yake katika kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi wake na pia kuhamasisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto hii muhimu.

Mkutano huu wa kimataifa umekusanya watu zaidi ya 1000, wakiwemo Marais, viongozi mbalimbali, asasi za kiraia, watu mashuhuri wenye ushawishi katika masuala ya nishati safi, na wadau wengine.

Lengo kuu ni kuongeza uelewa kuhusu suala hili sio tu katika bara la Afrika, bali pia kuliweka katika muktadha wa kimataifa ili kuhamasisha mchango wa kimataifa kufanikisha azma hiyo.

Pamoja na hayo, mkutano huu unalenga pia kuandaa sera madhubuti na zinazotekelezeka kwa ajili ya nishati safi ya kupikia, pamoja na kuharakisha ushirikiano wa wadau katika suala hili.

Makadirio yanaonesha kwamba takriban dola za Kimarekani bilioni 4 zinahitajika kila mwaka ili kufanikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa Waafrika wote ifikapo mwaka 2030.

Mkutano huu umepangwa na kusimamiwa na Shirika la Nishati Duniani (IEA) na kufanyika nchini Ufaransa. Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha uongozi katika suala hili kama Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika, akionyesha dhamira ya Tanzania katika kufanikisha malengo ya nishati safi ya kupikia na kukuza maendeleo endelevu kwa wananchi wake.

Ukiachana na jitihada za kuhamasisha nishati safi kimataifa zinazofanywa na Mhe Rais, vile vile hapa nchini Serikali ya Awamu Sita imeanzisha mpango mkakati wa kuboresha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kwa msistizo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu, amedhamiria  kuhakikisha tunafikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ifikapo mwaka 2033.

Hatua hii inalenga kusaidia kupunguza matumizi ya nishati zisizokuwa salama ambazo mara nyingi pia si rafiki kwa mazingira na afya ya binadamu kama vile matumizi ya Kuni na Mkaa. Kupitia mpango huu, Serikali inakusudia kutoa msaada wa kiteknolojia, kifedha, na elimu ili kuhamasisha jamii kutumia vyanzo vya nishati safi kama vile gesi asilia, umeme, na nishati ya jua kwa ajili ya kupikia.

Hatua hii itasaidia si tu kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi bali pia kuboresha afya na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 8 tu ya Watanzania wanatumia nishati safi kwa kupikia, huku asilimia 63.5 wakitumia kuni na asilimia 26.2 wakitumia mkaa. Kwa kuzingatia hali hii, imefanya serikali kuongeza jitihada katika mpango thabiti wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kupikia ili kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2033.

Mpango huu unahusisha mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu faida za nishati safi, kusambaza teknolojia bora za kupikia kama vile mitungi ya gesi, na kutoa mafunzo kuhusu njia mbadala za kupikia zenye athari ndogo kwa mazingira. Vile vile, serikali inalenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, ambayo ni chanzo kikuu cha ukataji miti na uharibifu wa mazingira, huku ikiongeza upatikanaji na matumizi ya nishati safi, ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya ya binadamu.

Bado watanzania wengi wanapuuzia hatari zitokanazo na matumizi ya mkaa, lakini tunapaswa kutambua kuwa zipo Kemikali hatari zinazopatikana kwenye moshi wa mkaa na kuni, kama vile sulphur dioxide, nitrogen dioxide, na carbon monoxide, ambazo zinaleta madhara makubwa kwa afya ya binadamu. Baadhi ya madhara hayo ni pamoja na:

  1. Saratani ya koo na mapafu: Kemikali hizi zinaweza kusababisha uharibifu kwenye seli za mapafu na koo, na hatimaye kusababisha ukuaji wa seli za kansa.
  2. Mapafu kupata lengelenge: Kutokana na kuathiriwa kwa tishu za mapafu na kemikali hizi, mtu anaweza kuathiriwa na tatizo la lengelenge, ambalo linaweza kusababisha matatizo ya kupumua na hata kifo.
  3. Kifua kikuu: Moshi wa mkaa na kuni unaweza kuchangia kuenea kwa bakteria wa kifua kikuu, ambayo ni ugonjwa hatari wa kuambukiza.
  4. Kikohozi na vidonda kwenye mfumo wa upumuaji: Kemikali hizi zinaweza kusababisha uchafuzi wa mfumo wa upumuaji, kusababisha kikohozi, vidonda, na matatizo mengine ya afya ya mfumo huo.

Kwa kuzingatia madhara haya kwa afya ya binadamu, ni muhimu sana kuchukua hatua za kupunguza matumizi ya mkaa na kuni kwa kupikia na badala yake kutumia nishati safi na rafiki kwa mazingira.

Takwimu hizi pia zinaonesha athari hizi zinapelekea Kupotea kwa maisha ya watu 33,000 kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati hii chafu, hii inatufanya kuamini kuwa nishati hii ni janga la kiafya na kijamii hapa nchini. Ukiachana na hayo, ni vema kutambua kwamba wahanga wengi wa matumizi ya nishati chafu ya kupikia ni wanawake.

Kwa sababu, mara nyingi wanabeba mzigo mkubwa wa kupika na kushughulikia familia  majumbani, ambayo mara nyingi inahusisha kutumia nishati chafu kama vile kuni na mkaa. Kwa kuwa wanawake wako karibu zaidi na shughuli hizi za kifamilia, wanaathiriwa zaidi na madhara ya moshi wenye sumu unaotokana na nishati chafu ya kupikia. Hii inamaanisha kuwa hatari za magonjwa ya kupumua na matatizo mengine ya kiafya yanawaathiri kwa kiwango kikubwa.

Kuongezeka kwa idadi ya vifo na athari kwa wanawake ni ishara ya dharura ya kuchukua hatua za haraka kubadilisha mbinu za kupikia na kukuza matumizi ya nishati safi na endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *