KWA STAILI HII TANZANIA INAENDA KUBAKIA NA CHAMA KIMOJA.

Tanzania inaelekea kubakia na chama kimoja cha siasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa kutokana na kuyumba kwa vyama vya upinzani, hususan Chadema, ambacho kilitarajiwa kuwa chama kikuu cha upinzani. Hali hii inasikitisha, lakini ni ukweli, hasa katika dunia nchi zinaposhindana kuvutia wawekezaji, watalii, na kupiga hatua katika teknolojia, ni wakati huo  Chadema wao wamejikita zaidi katika maandamano na kuleta vurugu, badala ya kutoa hoja za maendeleo.

Ni kweli kuwa kuna hali ya sintofahamu nchini, hususan baada ya tukio la kutekwa na kuuawa kwa kada wa Chadema, Ally Kibao, ambalo liliwashtua Watanzania wote. Rais Samia Suluhu Hassan alilaani kitendo hicho na kuagiza uchunguzi wa kina ili wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria. Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Rais Samia alisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, na kila raia ana haki ya kuishi kwa amani, akisema Serikali yake haitavumilia vitendo vya kikatili kama hicho.

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi, naye alitoa kauli akienda mbali zaidi na kusema mauaji ya kada huyo huenda yalilenga kuidhoofisha Serikali, ili ionekane imeshindwa kusimamia usalama. Viongozi wa dini walijiunga katika kulaani kitendo hicho na kushikilia msimamo wa Rais, wakisisitiza umuhimu wa uchunguzi na kuchukua hatua madhubuti ili kumaliza kabisa matukio hayo.

Wakati hatua za uchunguzi zikichukuliwa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliamuru makada wa chama hicho kutoka maeneo yote ya nchi wakutane Dar es Salaam kwa maandamano ambayo alisema yanalenga kudai uwajibikaji wa Serikali. Alisema pia bado wanaomboleza kifo cha kada wao. 

Hata hivyo, hili si tukio la kwanza la aina hii kwa Chadema mwaka huu, kwani walijaribu kufanya maandamano wakati wa Siku ya Vijana Duniani huko Mbeya, wakikusanya makada wao kwa nia ya kuleta vurugu, mfano wa maandamano ya Kenya. Polisi waliwazuia maandamano hayo, yaliyokuwa na viashiria vya vurugu, lakini Chadema waliridhika kwa kuwa walipata nafasi ya kujadiliwa katika mitandao ya kijamii. Na sasa, maandamano ya Septemba 23 yanaonekana kama jambo kubwa kwa Mbowe na Chadema.

Najiuliza, je, Mbowe hana hoja za msingi za kumkabili Rais Samia Suluhu Hassan katika meza ya majadiliano? Rais Samia anasimamia uchumi ambao kwa mara ya pili mfululizo, mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yamevuka Dola za Marekani bilioni tano, sawa na takriban shilingi trilioni 18, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa katika historia ya Tanzania. Aidha, Rais Samia ameimarisha mazingira ya biashara yaliyosaidia kukuza uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China, kutoka thamani ya shilingi trilioni saba hadi kufikia shilingi trilioni 20 ndani ya miaka miwili tu. Je, ataweza kuzungumza nini na Mbowe, ambaye mawazo yake yapo kwenye maandamano ya Mbeya na maandalizi ya vurugu za Septemba 23?

Tafakari, Rais Samia anasimamia ujenzi wa kampasi kubwa za vyuo vikuu 14 nchi nzima, ili vijana watakaomaliza elimu ya msingi na sekondari bila malipo wapate fursa ya elimu ya juu yenye ujuzi wa kimataifa. Je, atazungumza nini na Mbowe, ambaye anawasukumia vijana hao kwenye maandamano yenye viashiria vya vurugu? Rais Samia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, amepeleka wahadhiri 1,100 katika vyuo vikuu vikubwa duniani, ambapo 623 wanasomea shahada za uzamivu na 477 shahada za umahiri. 

Lengo ni kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi wa kimataifa. Je, ataweza kuzungumza nini na Mbowe, ambaye mawazo yake ni juu ya kutumia wahitimu hao kwenye maandamano?

Hapa sijataja miradi ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya umeme (SGR), ambayo imewezesha Watanzania kusafiri kutoka Dar es Salaam kwa muda wa saa tatu na nusu badala ya saa nane. Inawezekana hata baadhi ya watakaokuja kufanya vurugu Dar es Salaam Septemba 23 watatumia treni hiyo. 

Ni Rais Samia huyu huyu ambaye amewezesha nchi kupitia Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHP) kuwa na ziada ya megawati 700, kitu ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya nchi. Kwa haya yote, Rais Samia atazungumza nini na Chadema?

Katika muktadha huu, tunaona kuwa Rais Samia anafanya kazi kubwa kuimarisha taifa, wakati Chadema inajikita zaidi katika maandamano na vurugu badala ya kutoa mchango chanya kwa maendeleo ya nchi.

Credit: Tanzania leo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *