Mcheza ngoma mzuri hujua muda wa kushuka jukwaani.” Msemo huu maarufu wa Profesa Patrick Loch Otieno (PLO) Lumumba, mwanafalsafa na mwanasheria mashuhuri wa Kenya, unakumbusha viongozi umuhimu wa kujitathmini na kuachia wengine nafasi. Profesa Lumumba mara kwa mara hutumia maneno haya kuwahimiza viongozi, hasa katika siasa, kutambua wakati sahihi wa kupisha kizazi kipya na kuwaachia wengine nao waonyeshe uwezo wao.
Kama vile manju (kiongozi wa kundi la ngoma) anavyoongoza kundi kwa weledi, kiongozi mwenye busara hutambua kuwa kila wakati na nafasi ya kila mtu huja na hukoma. Kuachia majukumu si alama ya kushindwa bali ni busara na ukomavu, kwani ni vyema kuondoka jukwaani ukiwa umewacha wazo au mradi kuendelea kuwa na maana kwa wengine na kwa kizazi kijacho.
Kwa sasa nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), chama ambacho kilisimama kama nguzo muhimu ya upinzani na kutoa changamoto kubwa kwa serikali katika uchaguzi wa mwaka 2015, kinakumbwa na changamoto za ndani.
Viongozi wa chama kama Freeman Mbowe, Tundu Lissu, na Godbless Lema ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kwa muda mrefu sasa wanakiona chama kikipitia mivutano na migawanyiko ambayo imeanza kudhoofisha mshikamano wake. Migawanyiko hii, inayojitokeza hadharani, inaacha picha kuwa chama kimepoteza nguvu ya umoja wake wa awali.
Katika mataifa yenye demokrasia thabiti, vyama vya upinzani vina nguvu na mshikamano wa ndani. CHADEMA, kama chama kikuu cha upinzani nchini, kinakabiliwa na ukweli kwamba kinahitaji kujipanga upya, ili kiendelee kuwa na ushawishi wa kisiasa. Ni wakati kwa viongozi wa chama kujiuliza:
Je, wanatetea maslahi ya watu au wamezama katika fikra binafsi zinazotishia kuondoa lengo kuu la chama? Ikiwa viongozi hawa wataendelea na minyukano ya ndani bila kurekebisha hali, kuna hatari kwamba watapoteza imani na ushawishi kwa wananchi.
Kujitathmini na kuruhusu wengine kushika nafasi ni ishara ya ubinadamu na busara. Kama msemo unavyosema, “mcheza ngoma mzuri hujua muda wa kushuka jukwaani.” Ni wakati mwafaka sasa kwa viongozi wa CHADEMA kufanya tafakuri ya kina, kutanguliza mbele maslahi ya chama na wananchi, na kutafuta njia bora za kurejesha mshikamano na nguvu ya upinzani nchini.
Kiongozi bora anapaswa kuondoka jukwaani akiwa na heshima ya kuwaachia wale wanaokuja nafasi ya kuendeleza na kutetea misingi ya demokrasia.
Credit Salehe Mohamed