Tarehe 19 Machi 2021, Rais Samia Suluhu Hassan aliapishwa rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kifo cha ghafla cha mtangulizi wake, Hayati Dk. John Magufuli. Leo, takriban miaka minne baadaye, ni wakati mwafaka wa kutathmini uongozi wake na kujibu swali muhimu: Je, Dk. Samia ametimiza ahadi alizotoa kwa Watanzania?

Hakuna shaka kwamba majibu yatakuwa tofauti kulingana na mtazamo wa kila mtu. Hata hivyo, kipimo halisi cha mafanikio ya kiongozi ni namna ambavyo utawala wake umeleta maendeleo kwa wananchi na kuboresha maisha yao.
Dk. Samia na Safari ya Kuinua Taifa
Dk. Samia alikabidhiwa nchi katika kipindi kigumu, ambapo siyo tu alikuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania, bali pia alichukua madaraka wakati taifa likiwa kwenye mshtuko wa kuondokewa na kiongozi wake. Aliwahi kukiri kuwa alihisi woga na wasiwasi, lakini aliwaahidi Watanzania kwamba “Hakuna kitakachoharibika, hakuna kitakachosimama—kazi iendelee!”

Je, kaulimbiu hiyo ya Kazi Iendelee imetekelezwa kwa vitendo? Hakika, tathmini ya utawala wake inaonyesha kuwa amesimamia maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali zinazoathiri maisha ya Watanzania moja kwa moja.
Sekta ya Elimu: Kufanikisha Fursa Kwa Wote
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, wanafunzi wote waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza wameanza kwa wakati mmoja, tofauti na awali ambapo waligawanywa katika awamu kutokana na uhaba wa miundombinu na rasilimali. Hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa wote.
Sekta ya Afya: Miundombinu na Huduma Zaimarishwa
Dk. Samia amewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya kwa kujenga na kuboresha zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa, pamoja na hospitali za rufaa. Serikali yake imeongeza bajeti ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, hivyo kuboresha huduma za afya kwa wananchi mijini na vijijini.

Maji Safi na Salama: “Kumtua Mama Ndoo Kichwani”
Moja ya ahadi kubwa za Rais Samia ilikuwa kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama, hasa vijijini. Leo, takwimu zinaonyesha kuwa huduma ya maji safi imefikia asilimia 75 kwa nchi nzima, huku juhudi zikiendelea kufikisha maji kwa asilimia 85 vijijini na 95 mijini.
Hapo awali, upatikanaji wa maji ulikuwa changamoto kubwa licha ya Tanzania kuwa na vyanzo vingi vya maji. Hata hivyo, chini ya uongozi wa Dk. Samia, miradi ya maji imeongezeka kwa kasi, ikiendelea kumaliza tatizo hilo la muda mrefu.

Miundombinu: Njia za Maendeleo Kufunguliwa
Miundombinu bora ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya taifa lolote. Serikali ya Rais Samia imeendelea kuboresha barabara, madaraja, viwanja vya ndege, na hata sekta ya usafirishaji kwa njia ya reli.
Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) umepiga hatua kubwa, ambapo sasa treni inafanya majaribio kati ya Dar es Salaam na Morogoro. Hatua inayofuata ni kuendelea na ujenzi wa reli hiyo hadi Mwanza, Kigoma, na maeneo mengine.
Sekta ya Kilimo: Kutoa Uhakika wa Chakula na Malighafi za Viwanda
Rais Samia amesisitiza mara kwa mara kwamba Tanzania inapaswa kutumia rasilimali zake ipasavyo, hususan ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo. Serikali yake imewekeza katika:
- Utafiti wa mbegu bora
- Uboreshaji wa huduma za ugani
- Kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara
- Kupanua kilimo cha umwagiliaji
Juhudi hizi zina lengo la kuhakikisha nchi ina chakula cha kutosha na vilevile kuongeza upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani.

Usambazaji wa Umeme: Nishati kwa Kila Kitongoji
Rais Samia ameweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha vijiji vyote vinapata umeme ifikapo 2025. Lengo lake si tu kufikisha umeme vijijini, bali kuhakikisha unawafikia hata wakazi wa vitongoji vidogo, ili kuwezesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yote ya Tanzania
Uongozi wa Dk. Samia na Heshima ya Tanzania Kimataifa
Chini ya uongozi wake, Tanzania imeimarisha mahusiano ya kidiplomasia, ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji wa kigeni na kuimarisha biashara za kimataifa. Amani na utulivu vimeendelea kuwa nguzo kuu, jambo linalofanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.
Kutokana na mafanikio haya, haishangazi kwamba wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM wamempitisha Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Methali isemayo “Usione vinaelea, vimeundwa” inadhihirika wazi katika uongozi wa Rais Samia. Maendeleo yanayoonekana leo siyo bahati mbaya, bali ni matokeo ya kazi kubwa, maono, na dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania.
Wakati majirani wa Tanzania wakikumbwa na migogoro ya kisiasa na kiusalama, Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani. Ndani ya mazingira haya thabiti, kaulimbiu ya Kazi Iendelee imeendelea kutekelezwa kwa vitendo, ikileta maendeleo yanayogusa maisha ya kila Mtanzania.

2025: Wakati wa Kuendeleza Mafanikio
Kwa misingi hii, Uchaguzi Mkuu wa 2025 siyo tu utakuwa fursa ya kidemokrasia, bali pia utaamua hatma ya safari ya maendeleo ya Tanzania. Wakati huo ukifika, Watanzania wataamua kama wanataka kuendeleza kazi iliyoanzishwa au la.
Kwa sasa, ukweli ni kuwa: Dk. Samia ameongoza kwa ufanisi, na Tanzania inaendelea kusonga mbele kwa kasi!