Mnamo Desemba 5, mwaka 2018, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitangaza rasmi kuanza kusikiliza kesi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya video maarufu kama Video Conferencing. Hii ilikuwa hatua ya kihistoria iliyolenga kuboresha utoaji wa haki nchini kwa kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA.
Kwa mfano, kesi ya kwanza ya aina hiyo ilisikilizwa kwa kumhoji shahidi aliyekuwa nchini Ufaransa kupitia video, jambo lililoonesha kuwa Tanzania imeamua kuendana na kasi ya dunia katika matumizi ya teknolojia kwenye mifumo ya haki.
Mwaka mmoja baada ya hapo, yaani 2019, Mahakama ya Rufani ilitangaza kusikiliza jumla ya kesi 60 kwa njia ya mtandao kuanzia Oktoba 9 hadi 16. Kesi hizi zilihusisha masjala mbalimbali kama Tabora, Mwanza, Bukoba na Mbeya, na zilisikilizwa na Majaji 17 tofauti wa Mahakama ya Rufani kwa njia ya Video Conference.
Lengo lilikuwa ni kuokoa muda, gharama na kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kusafiri mbali kufuata haki zao.
Leo tukiwa mwaka 2025, ni miaka takribani saba tangu mfumo huu uanze kutumika nchini. Hii inamaanisha kuwa kesi kusikilizwa kwa mtandao si jambo geni wala la kushangaza. Ni njia ya kawaida inayotambulika kisheria, na imeendelea kutumika kwa mafanikio makubwa.
Lakini kilichonishangaza ni kitendo cha mawakili wa upande wa mwanasiasa Tundu Lissu siku ya jana kugomea kusikiliza kesi kwa njia ya mtandao, kama vile hawajawahi kusikia wala kushuhudia mfumo huu ukitumika.
Kitu hiki kimenifanya niamini kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanatafuta huruma ya umma kwa kulazimisha drama isiyo na msingi, badala ya kuendana na taratibu zinazotambuliwa na mahakama.
Ni muhimu tukumbuke kuwa ni mamlaka ya mahakama kuamua namna bora ya kuendesha kesi. Kama njia ya mtandao imeonekana inafaa na inatumika kwa maelfu ya kesi nyingine nchini bila malalamiko, haipaswi kufanywa suala la kisiasa au la kutafuta umaarufu.
Wenzetu wanapiga hatua mbele kwa kutumia teknolojia kutatua changamoto, sisi bado tunataka tuone kamera na waandishi wa habari kila kona ili kuendelea kutengeneza propaganda ambazo hazina manufaa kwa ukuaji wa nchi.
Ukweli ni kuwa huu si wakati wa kuigiza bali wa kila mmoja kusimama kwenye nafasi yake wanasiasa, mawakili, mahakama na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa ufanisi na utulivu.
Tuache kutafuta ushujaa na kutia huruma kwa mambo madogo. Tujikite kwenye kazi. Teknolojia si adui wa haki bali ni nyenzo ya kutusaidia kama mnavyotumia kutoa updates mitandaoni za matukio yanayowakuta.
Na kama taifa, hatupaswi kurudi nyuma kwa sababu ya kelele za watu wachache. Tuendelee kusimama imara kwa ajili ya maendeleo na haki ya kweli kwa wote.