RAIS SAMIA World Justice Project - WJP RAIS SAMIA World Justice Project - WJP

TANZANIA YAONGEZA VIWANGO VYA UTAWALA WA SHERIA DUNIANI: HALI YA NCHI KIDUNIA

Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imepiga hatua kubwa kuelekea mfumo wa kisheria unao wajibika zaidi, wenye uwazi, na haki.

Ripoti ya 2024 ya Mradi wa Haki Duniani (World Justice Project – WJP) kuhusu Utawala wa Sheria imetambua jitihada hizi, ikionesha kupanda kwa Tanzania kwenye viwango vya utawala wa sheria kimataifa.

Mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya Rais Dkt. Samia katika kujenga mfumo thabiti wa utawala unaozingatia misingi ya haki na usawa kwa kila raia.

Katika Ripoti ya Utawala wa Sheria ya 2024 ya Mradi wa Haki Duniani (WJP), Tanzania ilipata alama ya 0.47 na ilishika nafasi ya 96 kati ya nchi 142.

Hii ni ongezeko la alama 0.2% kutoka mwaka uliopita, ishara kwamba Tanzania imepata mafanikio katika baadhi ya maeneo yanayohusiana na utawala wa sheria. 

Tumepanda juu kulinganisha na mwaka 2021, ambapo Tanzania ilishika nafasi ya 100 kati ya nchi 139 kwenye Kielezo cha Utawala wa Sheria cha World Justice Project (WJP).

Nafasi hii iliweka Tanzania kwenye kiwango cha chini kimataifa, lakini hali hii ililingana na mwelekeo wa mataifa mengi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kati ya nchi zenye kipato cha chini-kati. 

Kielezo cha Utawala wa Sheria hupima nchi kwa vigezo kadhaa, ikiwemo uwajibikaji wa serikali, kutokuwepo kwa rushwa, uwazi wa serikali, haki za msingi, amani na usalama, utekelezaji wa sheria, na haki za kiraia. 

Muhtasari wa Utendaji wa Tanzania Kwenye Kielezo cha Utawala wa Sheria cha World Justice Project

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopimwa kila mwaka na Kielezo cha Utawala wa Sheria cha “World Justice Project (WJP)”, kielezo kinachozingatia vigezo mbalimbali vinavyopima ubora wa utawala, ufanisi wa mfumo wa haki, na uhifadhi wa haki za binadamu baadhi ya vipimo vinaonesha kuwa. 

Kikwazo kwa Mamlaka ya Serikali (0.50)

Tanzania imepata alama ya 0.50 katika kipengele hiki, ambayo inaashiria hatua za uwajibikaji zilizopo, ingawa bado kuna haja ya kuimarisha mfumo wa kudhibiti mamlaka za serikali.

Kwa alama hii, Tanzania iko juu kidogo ya wastani wa kikanda (0.46), lakini bado iko chini ya wastani wa kimataifa (0.54). Hii inaonyesha kuwa kuna mifumo ya uwajibikaji, lakini inahitaji maboresho ili kuleta usawa zaidi katika utawala wa serikali.

Kutokuwepo kwa Rushwa (0.41)

Katika kipengele cha kutokuwepo kwa rushwa, Tanzania imepata alama ya 0.41, ambayo iko juu ya wastani wa kikanda (0.38) lakini chini ya wastani wa kimataifa (0.51).

Alama hii inaonyesha kuwa ingawa kuna juhudi katika kupambana na rushwa, bado kuna changamoto kubwa katika sekta ya umma, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vibaya ya fedha na rasilimali za umma. Hivyo, bado kuna umuhimu wa kuongeza juhudi za kupambana na rushwa.

Amani na Usalama (0.70)

Hii ni moja ya maeneo ambayo Tanzania imefanya vizuri, ikipata alama ya 0.70, ambayo ni juu ya wastani wa kikanda (0.62) na karibu na wastani wa kimataifa (0.72).

Ufanisi katika kudumisha amani na usalama inaonesha juhudi za serikali katika kukabiliana na uhalifu na kuhakikisha usalama wa raia. Hata hivyo, bado kuna nafasi ya kuboresha zaidi mifumo ya usalama ili kufikia viwango vya kimataifa.

Utekelezaji wa Sheria (0.46)

Alama ya 0.46 katika utekelezaji wa sheria inaonyesha kuwa Tanzania inafanya vizuri kidogo kulinganisha na wastani wa kikanda (0.45).

Japokuwa, kuna changamoto katika utekelezaji wa sheria kwa usawa na ufanisi, na hii inahitaji marekebisho ili kuhakikisha kuwa sheria zinaheshimiwa na zinatekelezwa kwa usawa.

Haki za Kiraia (0.48)

Katika kipengele cha haki za kiraia, Tanzania inapata alama ya 0.48, ikiwa juu kidogo ya wastani wa kikanda (0.47). Hii inaonyesha upatikanaji wa haki za kiraia, ingawa bado kuna changamoto zinazohusiana na ucheleweshaji na upendeleo katika utoaji wa haki.

Tanzania inaonekana kufanya vizuri katika maeneo ya Amani na Usalama na Kikwazo kwa Mamlaka ya Serikali, Katika maeneo mengine, kama vile utekelezaji wa sheria na haki za kiraia, Tanzania inaonyesha maendeleo lakini bado inakutana na changamoto zinazohitaji mikakati ya kisasa ya kuboresha mifumo ya sheria na usimamizi wa haki.

Serikali ya awamu ya sita imechukua hatua mbalimbali za kudhibiti na kupambana na ufisadi, hatua ambazo zimeimarisha heshima ya kimataifa ya Tanzania.

Kwa msisitizo wa uwazi na uwajibikaji, Rais Dkt. Samia ameonyesha kuwa serikali yake inajitahidi kuhakikisha kuwa vitendo vya ufisadi haviwezi kudhoofisha maendeleo ya taifa.

Huu ni ujumbe thabiti kwa Watanzania na jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania iko tayari kwa kasi ya maendeleo endelevu inayojikita katika maadili ya haki na uadilifu.

Pamoja na kuimarisha mapambano dhidi ya ufisadi, Rais Dkt. Samia ameanzisha mageuzi makubwa katika sekta ya sheria yanayolenga kuboresha na kulinda haki za Watanzania.

Moja ya maeneo ya kipaumbele ni kuimarisha taasisi za ndani na kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu katika masuala ya utawala. Hatua hizi zimeleta usawa katika jamii kwa kutoa fursa sawa kwa kila Mtanzania kunufaika na mfumo wa sheria unaojali haki na uwajibikaji.

Zaidi ya hayo, uongozi wa Rais Dkt. Samia umeweka mazingira bora kwa uhuru wa mahakama, ukionesha juhudi za kukomesha ushawishi wa kisiasa. Mahakama isiyo na upendeleo inadhihirisha jitihada za Rais kuhakikisha kuwa haki za msingi na uhuru wa wananchi zinalindwa, bila kuingiliwa na maslahi ya kisiasa.

Watanzania wanashuhudia kwa macho yao mageuzi haya makubwa, yanayoonekana kuwa muhimu kwa mustakabali bora na wa kidemokrasia wa taifa.

Licha ya changamoto za ulimwengu zinazokabili taifa, hatua hizi za Rais Dkt. Samia zimezidi kuwavutia na kuwapa matumaini Watanzania na mataifa mengi ambayo yanaiona Tanzania mpya inayowajibika, yenye uadilifu na inayoweka maslahi ya wananchi mbele.

Dunia imetambua jitihada hizi, na kupanda kwa Tanzania katika viwango vya Ripoti ya Utawala wa Sheria ya WJP ni ushahidi kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuacha urithi wa maendeleo endelevu, haki, na uwajibikaji kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kadiri Tanzania inavyoendelea kupanda kwenye viwango vya kimataifa, ni wazi kuwa Rais Dkt. Samia anajenga taifa lenye msingi imara wa utawala bora unaoambatana na maadili ya kisasa ya demokrasia, uhuru wa raia, na utawala wa sheria. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *