Makamu mwenyekiti Tundu Lissu Asisimua Wanachama, Lakini Mbegu za Mgawanyiko Zaanza Kuonekana
Katika hatua ya kusisimua lakini pia yenye kuibua mijadala mikali, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Tundu Antipas Lissu, ametangaza nia yake wazi rasmi ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Taifa wa CHADEMA.
Tangazo hili limepokelewa kwa shangwe na matumaini miongoni mwa baadhi ya wanachama walioudhuria katika mkutano huo, lakini pia na wale ambao walikuwa wakitamani mabadiliko ya muda mrefu katika chama hicho baada ya kuchoshwa na utawala wa mwenyekiti aliyekaa madarakani kwa muda mrefu.
Katika mkutano uliowakutanisha wanahabari na wanachama kadhaa, Lissu ametangaza rasmi azma yake ya kuwania nafasi ya juu ya uongozi wa CHADEMA, akisisitiza umuhimu wa mabadiliko na ukomo wa madaraka.
Lissu ameongeza kuwa, mfumo wa sasa wa chama hicho ambao unaegemea kumtegemea mtu mmoja ni wa hatari hususani kwa maendeleo endelevu ya chama na unaweza kusema pia ni hatari kwa chama kinachojiita cha kidemokrasia.
Mbegu za Mgawanyiko: Wanachama Wako Kambi Mbili
Ingawa Lissu ameibuka na kauli zake siku ya leo, kama kiongozi wa mwongoza njia kwa wale wanaotamani mabadiliko ya muda mrefu, hali ya mshikamano wa CHADEMA imeanza kuonekana kuwa na nyufa.
Wakati wanachama wa kawaida wakionekana kuhamasishwa na hotuba zake, baadhi ya viongozi wakuu wamekuwa hawaonekani wazi katika hotuba zake, wala kumuunga mkono hadharani sawa na inavyokuwa kwenye hotuba za mwenyekiti wa chama.
Na hizi ndio Taarifa za ndani zinaonyesha kuwa mgawanyiko huu tayari umeanza kufifisha mshikamano wa chama kuelekea uchaguzi wa ndani kama aliyowahi kusema kada wa zamani wa chama hicho Mchungaji Peter Msigwa.
Na sasa Wanachama wengi wameanza kugawanyika katika makundi mawili makuu:
- Kambi ya Mabadiliko: Inayoongozwa na wafuasi wa Lissu, wanaodai kuwa ukomo wa madaraka ni msingi wa demokrasia na maendeleo. Wanachama hawa wandai wanataka kukomesha vitendo vya uchawa ndani ya CHADEMA na matumizi mabaya ya nafasi za uongozi na vitendo vya rushwa vilivyogubika chaguzi za chama hicho.
- Kambi ya Mwenyekiti: Inajumuisha wale wanaotetea uongozi wa sasa, wakiamini kuwa utulivu wa chama umetokana na uzoefu na uongozi wa Freeman Mbowe, ambaye ameiongoza CHADEMA kwa zaidi ya muongo mmoja.
Hatari ya Mpasuko Mkubwa
Mgawanyiko huu si tu kwamba unatishia mshikamano wa CHADEMA, bali pia unatoa nafasi kwa wapinzani wa kisiasa kuendelea kukua na kujiimarisha kuekelea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na Endapo Lissu hatashinda uchaguzi wa uenyekiti, kuna hatari kubwa ya wafuasi wake kuona mchakato mzima wa uchaguzi kama wa udanganyifu, kutokana na mwenyekiti kuushikilia mfumo mzima, hali ambayo inaweza kusababisha upinzani wa ndani na hata kujiondoa kwa baadhi ya wanachama muhimu.
Kwa upande mwingine, iwapo Mbowe ataendelea kushikilia nafasi ya uenyekiti, kambi ya wafuasi wa mabadiliko inaweza kuhisi kusalitiwa, na hivyo kuchochea upinzani wa wazi au wa kimyakimya dhidi ya maamuzi ya chama.
Tayari Lissu ameonyesha dalili za kutoridhishwa na vitendo vya uchaguzi ndani ya CHADEMA, akitaja udanganyifu na matumizi ya pesa chafu kama tatizo linalohitaji kushughulikiwa haraka.
Je, CHADEMA Itaweza Kusimama Imara?
Kwa hali ilivyo hivi sasa, uchaguzi wa ndani wa CHADEMA unatarajiwa kuwa kipimo kikubwa cha mshikamano wa chama hiki. Kama Lissu alisema katika hotuba yake, “Muda wa kushangilia unakuja.”
Je, wanachama wa CHADEMA wataweza kushangilia pamoja kama familia moja baada ya uchaguzi huu, au watajikuta wakigawanyika zaidi?
Ni dhahiri kuwa mwelekeo wa uchaguzi huu wa ndani utatoa picha halisi ya mustakabali wa chama hiki kikuu cha upinzani.
Muda utaamua kama CHADEMA itajifunza kutoka kwa changamoto hizi na kuibuka imara zaidi, au kama mgawanyiko huu utasambaratisha misingi iliyojengwa kwa miaka mingi.