TUNDU LISSU HAFURAHISHWI NA CHADEMA YA SASA

Fununu zimeibuka zikidai kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Tundu Lissu, ametoa kauli nzito zinazozua mjadala kuhusu mustakabali wa chama hicho.

Ujumbe unaodaiwa kuwa wake, uliosambazwa kupitia kundi la WhatsApp linalohusishwa na wanachama wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, unaonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu mwelekeo wa chama hicho, hasa katika mazingira ya sasa ya kisiasa nchini Tanzania.

Katika ujumbe huo, inadaiwa kuwa ujumbe wake katika kundi hilo la la wanachama wa CHADEMA Kaskazini, Lissu ameonekana kupinga dhana ya kushiriki kila uchaguzi bila mabadiliko ya msingi katika mfumo wa uchaguzi. Ameonya kwamba kushiriki uchaguzi chini ya mfumo wa sasa kunaweza kudhoofisha chama na kusababisha kupoteza imani ya wanachama na wafuasi wake. Alieleza:

“Chama cha siasa chenye malengo ya kushika dola ili kufanya mabadiliko ya msingi katika siasa, uchumi, na jamii lazima kipiganie kwanza mabadiliko ya msingi ya mfumo wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki. Kikikosa kufanya hivyo, kitakufa kifo cha asili.”

Mifano ya Kihistoria

Katika ujumbe huo, Lissu alitaja mifano ya vyama vya siasa vya kihistoria barani Afrika ambavyo vilikataa kushiriki uchaguzi hadi pale mabadiliko ya msingi yalipofanyika. Alitaja ANC ya Afrika Kusini, ambayo haikushiriki uchaguzi wowote hadi Katiba Mpya ya kidemokrasia ilipopitishwa mwaka 1996, na ZANU-PF ya Zimbabwe chini ya Robert Mugabe, ambayo ilikataa kushiriki uchaguzi hadi ilipopatikana Katiba ya Uhuru mwaka 1980.

Kwa upande mwingine, Lissu alikosoa vyama kama UDP ya John Cheyo na CUF ya Prof. Ibrahim Lipumba, ambavyo vilishiriki uchaguzi usio wa haki na hatimaye kupoteza ushawishi wao. Alisema kuwa vyama vinavyoshiriki uchaguzi bila mabadiliko ya msingi hukubali na kuhalalisha kasoro zilizopo, hali inayoweza kusababisha wananchi kukata tamaa na chama kupoteza umaarufu.

Migawanyiko Ndani ya CHADEMA

Fununu hizi zimeibuka wakati ambapo CHADEMA inakabiliwa na changamoto mbalimbali za ndani, zikiwemo tuhuma za rushwa na migawanyiko miongoni mwa wanachama. Taarifa zinadai kuwa baadhi ya viongozi wa ngazi za mikoa wamekuwa wakihama kimyakimya, huku wengine wakihusishwa na mapambano ya madaraka yanayosababisha migogoro waziwazi.

Hali hii imejidhihirisha hivi karibuni katika vurugu zilizotokea kwenye uchaguzi wa viongozi wa chama Mkoa wa Arusha, ambapo wanachama waliripotiwa kuchapana ngumi hadharani. Tukio hilo limezua maswali kuhusu mshikamano wa chama na uwezo wake wa kudhibiti changamoto za ndani.

Kauli ya Lissu: Mapambano ya Kweli

Katika ujumbe huo, Lissu anadaiwa kuhimiza wanachama wa CHADEMA kusimama kidete kwa ajili ya mapambano ya mabadiliko ya kweli. Alisisitiza kuwa Katiba Mpya ya kidemokrasia haiwezi kupatikana bila juhudi za makusudi na mapambano ya dhati. Alisema:

“Katiba ya kidemokrasia ya wananchi itapiganiwa. Haitatolewa kwenye beseni! Ni mapambano mbele kwa mbele mpaka kieleweke.”

Aidha, alitoa changamoto kwa wanachama kuamua kama wanataka CHADEMA ibaki kuwa chama cha mapambano ya kweli au kufuata nyayo za vyama vilivyopoteza mwelekeo kwa kushiriki kila uchaguzi bila masharti. Alifafanua kuwa uchaguzi wa 2019, 2020, na 2024 unapaswa kuwa funzo kwa CHADEMA kuhusu aina ya changamoto zinazoikabili nchi katika mfumo wa uchaguzi.

Mustakabali wa CHADEMA

Ingawa fununu hizi bado hazijathibitishwa rasmi na uongozi wa CHADEMA, mjadala umekuwa mkubwa miongoni mwa wanachama na wafuasi wa chama hicho. Wengi wanaonekana kushangazwa na maudhui ya ujumbe huo, huku wengine wakiona ni mwito wa kuimarisha msimamo wa chama.

Je, CHADEMA itaweza kushinda changamoto hizi za ndani na kuendelea kuwa sauti ya upinzani yenye nguvu nchini? Fununu hizi zinaacha maswali mengi ambayo bado hayajajibiwa rasmi, lakini ukweli utaonekana kadri muda unavyosonga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *